Serikali ya Tanzania imetangaza kuunda kamati ya pamoja ya wataalam bara na visiwani itakayoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kupitiwa upya usajili uliokwishafanyika na kuzihakiki taarifa za meli zote zilizosajiliwa nchini, kuangalia mwenendo mzima wa usajili, na hatimaye kutoa mapendekezo na ushauri kwa Serikali.

Hatua hiyo inachukuliwa baada ya taarifa ya kukamatwa kwa meli zilizokuwa zimepakia shehena za dawa za kulevya na silaha zikiwa zinapeperusha bendera ya Tanzania.
Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akitoa taarifa kwa vyombo vya habari na umma juu ya hatua zinazochukuliwa na kukamatwa kwa meli hizo za Kaluba yenye usajili namba IMO 6828753 iliyokamatwa mwishoni mwa mwaka jana na wastani wa kilo 1,600 za dawa za kulevya katika maeneo ya Jamhuri ya Dominican Republic; na
Andromeda yenye namba za usajili IMO 7614666 iliyokamatwa ikisafirisha silaha kinyume na Sheria za kimataifa.
Makamu wa Rais amefahamisha kuwa Tanzania ilitoa kibali kwa kwa Jeshi la Mwambao wa Marekani na Jeshi la Mwambao wa Ugiriki kuweza kuzikamata na kuzipekua meli hizo.
Na baada ya upekuzi, hatua za haraka zilizochukuliwa na Tanzania ni kufuta Usajili wa Meli hizo.
Makamu wa Rais amesema piua taarifa za kukamatwa kwa meli hizo zimeleta mshtuko mkubwa ndani ya nchi, kutokana na kwamba Tanzania imejipambanua kupambana na maovu hayo kwa nguvu zake zote.
Meli hizo mbili zilisajiliwa Tanzania kupitia taasisi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar ambayo ndiyo imepewa mamlaka ya kusajili meli za nje.
Usajili wa Meli za Nje hufanywa na nchi nyingi duniani, ambapo Afrika nchi zinazofanya usajili wa kimataifa ni pamoja na Liberia, Komoro na Sierra Leone. Aidha, kwa Bara la Asia, ni pamoja na China na Singapore. Na Amerika ya Kusini ni pamoja na Panama.
Aidha imebainika kuwa wenye Meli hupendelea kusajili meli zao nje ya nchi zao kwa kukimbia uzito wa kodi na sheria zinazobana shughuli zao.