Muonekano wa tuta la kutandazia reli ya kisasa (Standard Gauge) katika eneo la Soga mkoa wa Pwani takriban kilomita 37 kutoka Pugu mkoa wa Dar es salaam ulivyo sasa unaridhisha.
Hii ni hatua iliyofikiwa katika muendelezo wa ujenzi wa reli hiyo ulioanza mwezi Desemba mwaka jana katika mradi unaotarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu na utajengwa kwa awamu nne.
Kampuni Hodhi ya rasilimali za reli nchini (RAHCO) ndiyo inatekeleza mradi huo kutoka Dar es salaam kwenda Isaka na Mwanza imegawanyika katika awamu ndogo nne ikiwemo Dar es salaam hadi Morogoro, Morogoro hadi Makutupora, Makutupora hadi Tabora na Tabora hadi Mwanza.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa RAHCO Injinia Masanja Kadogosa jumla ya makandarasi wanne wanaendelea na kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi wa reli hiyo yenye upana wa mita 1.345 na ambao utaruhusu treni kutembea kwa spidi ya kilomita 160 kwa saa.
Mradi huu mkubwa unatarajiwa kuchochea maendeleo katika sekta ya kilimo, biashara, madini na viwanda hususan maeneo ambapo reli hiyo itapita ikiwemo nchi jirani ya Rwanda ambayo imekubali kujenga aina hiyo ya reli toka Isaka hadi Kigali. Mtandao mzima wa reli nchini unaotegemewa kujengwa kwa kiwango cha standard Gauge una jumla ya kilometa 2,561 ukitarajiwa kugharimu Dola za Marekani Bilioni 7.683.
|
0 Comments