Daktari mmoja nchini Kenya amewasilisha kesi mahakamani akitaka upashaji tohara wa wanawake ambao hufahamika pia kama ukeketaji uhalalishwe.
Dkt Tatu Kamau anasema sheria inayoharamisha ukeketaji wa wanawake na wasichana inakiuka utamaduni katika jamii nyingi za Kiafrika.

kadhalika, amesema ni ubaguzi dhidi ya wanawake ikizingatiwa kwamba upashaji tohara wa wanaume unakubalika kisheria.
Daktari huyo anataka pia bodi ambayo iliundwa nchini humo kukabiliana na upashaji tohara wa wanawake ivunjiliwe mbali.
Aliwasilisha kesi hiyo katika Mahakama Kuu mjini Machakos, mbele ya jaji David Kemei.
Kesi hiyo itaanza kusikilizwa mwezi ujao.
Dkt Kamau, akizungumza na wanahabari baada ya kuwasilisha kesi yake, alisema wanawake wote, sawa na watu wazima popote pale, wanafaa kuruhusiwa kufanya uamuzi kuhusu miili yao wenyewe bila kuwekewa vikwazo na sheria.
Amesema ukeketaji ni neno ambalo lilitetwa na watu kutoka nchi za Magharibi
Lakini sasa amesema raia wa nchi za Magharibi wanafanya jambo sawa na ukeketaji, kufanya upasuaji kwenye uke kurekebisha maumbile.
"Upashaji tohara ulikuwa sehemu ya utamaduni wa Waafrika kabla ya kufika kwa wakoloni na haifai kuharamishwa," amesema.
"Punde tu itakapohalilishwa, tutaweza kufanya tohara kwa njia iliyo bora Zaidi, mojawapo ikiwa njia ya hospitali. Tukifanya hivyo basi itakuwa salama kabisa. Na njia hii ni mojawapo wa upasuaji wa kawaida duniani kote."
Wanawake wakiandamana dhidi ya ukeketaji wa wasichana Nairobi awali 23 January 2007 KasaraniHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Image captionWanawake wakiandamana dhidi ya ukeketaji wa wasichana Nairobi awali
Anasema wanawake wengi wamekuwa wakisumbuliwa na maafisa wa dola au hata kufungwa jela kwa sababu ya ukeketaji.
"Ingawa tunataka sana kumlinda mtoto msichana, kuna wanawake wengi sana ambao wamekamatwa na kufungwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita," anasema.
"Unapokuwa mtu mzima, hakuna sababu yoyote ya kuzuia kufanya uamuzi (iwapo ungependa kupashwa tohara)" alisema.

Takwimu muhimu kuhusu ukeketaji Kenya

  • Asilimia 21 ya wanawake wa umri wa kati ya miaka 15-49 Kenya wamepashwa tohara
  • Kuna ushahidi kwamba siku hizi, wasichana wamekuwa wakikeketwa wakiwa na umri mdogo. Asilimia 28 ya wanawake wa miaka 20-24 walikeketwa wakiwa na miaka 5-9, ikilinganishwa na asilimia 17 ya wanawake wa miaka 45-59.
  • Kuhusu aina ya ukeketaji, asilimia 2 ya wanawake wa miaka 15-49 hawakutolewa sehemu yoyote kwenye uke wao, asilimia 87 walikatwa na kuondolewa sehemu fulani, nao asilimia 9 walikatwa kisha kushonwa.
  • Wasichana wa miaka 0-14 wana uwezekano wa juu wa kukeketwa ikiwa mama zao wamekeketwa.
  • Wanawake na wanaume asilimia 11 huamini kwamba ukeketaji unahitajika kwa mujibu wa jamii yao au dini na kwamba unafaa kuendelea.
Chanzo: Takwimu ya Utafiti kuhusu Afya na Watu Kenya ya mwaka 2014

Dkt Kamau alisema jamii nyingi zimekuwa zikifanya upashaji tohara kwa njia nyingi na kwamba si aina zote za tohara hiyo ambayo ina madhara kwa mwanamke.
Alisema sawa na jinsi watu huonywa dhidi ya athari za uvutaji sigara au ungwaji pombe, kampeni ya kuwahamasisha watu kuhusu madhara ya ukeketaji inafaa kuendelea lakini wale wanaoamua au wangependa kupashwa tohara wanafaa kuruhusiwa.
Mamilioni ya wanawake duniani wamekeketwaHaki miliki ya pichaALAMY
Image captionMamilioni ya wanawake duniani wamekeketwa
Dkt Kamau ameshutumu hatua ya Bunge nchini Kenya la kupitisha sheria ya kuharamisha ukeketaji akisema Bunge lilivuka mipaka na kuingilia masuala ya utamaduni.
"Iwapo wanaweza kuharamisha utamaduni, kesho wataharamisha dini au kitu kingine. Dada anastahili kutetewa akifanya maamuzi yake, na wala si kulazimishwa kufanya mambo mengine," amesema.
Makundi yanayokabiliana na ukeketaji yameshutumu hatua ya Dkt Kamau.
Mwenyekiti wa bodi ya kukabiliana na ukeketaji Bernadette Loloju amesema ukeketaji hupingwa kwa sababu ya madhara yake kwa wanawake, hasa wakati wa kujifungua.
Amesema kampeni hiyo imefanikiwa kupunguza visa vya ukeketaji kutoka asilimia 37 mwaka 2008 hadi 21 mwaka 2014 kwa mujibu wa takwimu za serikali.
Kwa sasa hata hivyo, ukeketaji hutekelezwa kisiri.
Watoto wamekuwa pia wakipashwa tohara wakiwa wadogo kinyume na zamani ambapo ulifanywa wasichana wakibalehe.
Wasichana takriban 140 milioni wamekeketwa maeneo ya Afrika, Mashariki ya Kati na Bara Asia.
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo pia zimeathiriwa pakubwa na ukeketaji wa wasichana.
Inakadiriwa kwamba nchini Tanzania, wasichana na wanawake 7.9 milioni wamekeketwa.

Kwa nini imekuwa vigumu kukabiliana na ukeketaji?

Katika baadhi ya jamii Afrika Mashariki, ni utamaduni unaoathiri hadhi ya mwanamke katika jamii. Baadhi ya jamii, mwanamke haruhusiwi kuolewa au kutangamana na wasichana wengine wa rika lake iwapo hatapashwa tohara.
Katika jamii ya Wamaasai kwa mfano, mwanamke huwa na wakati mgumu kuthibitisha kwamba yeye ni mwanamke kamili iwapo hajapashwa tohara.
Aidha, watoto wake huchukuliwa na jamii kama wasiokubalika.
Sherehe ambazo huambatana na upashaji tohara na wazazi wa msichana kutambuliwa kama wazee katika jamii iwapo binti mabinti wao wamepashwa tohara huwafanya kutaka sana mabinti wao wakeketwe.