Na Jumia Travel Tanzania




Idadi ya watalii duniani imekuwa kwa kiwango cha 7% mwaka 2017 na kufikia idadi ya milioni 1,322, kwa mujibu wa matokeo ya hivi karibuni yaliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UNWTO).


 




Kulingana na takwimu zilizoripotiwa kutoka sehemu tofauti duniani, inakadiriwa kwamba idadi ya watalii waliowasili duniani kote imeongezeka kwa 7% mwaka 2017. Hii ni ishara nzuri au zaidi ya kiwango kilichokuwepo cha 4% kilichodumu tangu mwaka 2010, hivyo kuonyesha matokeo mazuri ndani ya miaka saba. 


Kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwa Afrika ambazo Jumia Travel ingependa kukushirikisha, ukuaji katika mwaka 2017 ulikadiriwa kuwa wa 8%. Ilijiimarisha kama ilivyokuwa kwa mwaka 2016 na kuwa na matokeo mazuri yaliyofikia idadi ya watalii milioni 62 kutembelea kutoka mataifa tofauti duniani. Licha ya changamoto mbalimbali hususani za kisiasa, nchi za Kaskazini mwa Afrika zilirejea kuwa na matokeo mazuri kwenye sekta ya utalii ambapo idadi ilikuwa kwa 13%, wakati nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara zenyewe idadi iliongezeka kwa 5%.


Mwaka 2017 ulitawaliwa na ukuaji endelevu kwenye maeneo mengi na kwa maeneo yaliyokumbwa na changamoto miaka iliyopita yaliimarika na kurejea hali zao za kawaida. Kwa kiasi kikubwa matokeo haya yamepelekewa na mabadiliko kwenye uchumi wa dunia na uhitaji mkubwa kutoka kwenye nchi nyingine na masoko mapya ya kitalii, hususani kuongezeka kwa matumizi makubwa kwenye nchi kama vile za Brazili na Urusi ambazo kwa miaka michache iliyopita zilikuwa zimeshuka kidogo. 


“Utalii wa kimataifa unaendelea kukua na thabiti, na kuifanya sekta ya utalii kuwa imara katika kuendesha shughuli za maendeleo ya uchumi. Ikiwa ni sekta ya tatu katika kuleta mapato ya kigeni duniani, utalii ni muhimu katika kutengeneza ajira na ustawi wa jamii duniani kote,” alisema Katibu Mkuu wa UNWTO Bw. Zurab Pololikashvili kwenye taarifa hiyo. “Bado tukiendelea kukua lazima tufanye kazi kwa kushirikiana ili kuhakikisha kwamba ukuaji huu unainufaisha kila jamii kwenye eneo walilopo, na tunakuwa sambamba kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu.” 


Ukuaji unatarajiwa kuendelea kwa mwaka 2018 


Kasi ya ukuaji imara uliopo hivi sasa inatarajiwa kuendelea mwaka 2018, tena katika kasi endelevu zaidi baada ya miaka 8 ya upanuzi wa kutosha kufuatia changamoto za kiuchumi na fedha mwaka 2009. Kulingana na mienendo ya sasa, matarajio ya kiuchumi na mtazamo kutoka kwa jopo la wataalamu wa UNWTO, UNWTO inatazamia idadi ya watalii kimataifa kwenye maeneo mbalimbali duniani kukua katika kima cha 4% mpaka 5% mwaka 2018. Kwa kiasi fulani hii ni juu kwa 3.5% ya ongezeko la wastani wa kawaida uliotazamiwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 mpaka 2020 na UNWTO katika utabiri wake wa Utalii Kuelekea 2030. Ulaya na Amerika zote zinatarijiwa kukua kwa 3.5% mpaka 4.5%, Asia na Pasifiki kwa 5% mpaka 6%, Afrika kwa 5% mpaka 7% na Mashariki ya Kati kwa 4% mpaka 6%.


 


Utalii Tanzania katika mwaka 2017





Mwaka 2017 ulikuwa ni wenye neema na mafanikio kwa upande wa Tanzania kwani ilishuhudia matukio makubwa kama vile kuja kwa watu mashuhuri kutembelea vivutio vya kitalii kama vile; Will Smith (mwanamuziki na mcheza filamu), David Beckham (aliyekuwa mcheza soka wa vilabu vya Manchester United, Real Madrid, AC Milan na PSG), Mamadou Sakho (aliyekuwa mchezaji wa Liverpool), Morgan Schneiderlin (mchezaji wa Everton) pamoja na ziara ya kikosi kizima cha timu ya Everton kutokea ligi kuu ya Uingereza.





Ujio wa watu hao mashuhuri nchini Tanzania ulisaidia kuipaisha sekta ya utalii kwani katika matembezi yao waliweza kushirikisha dunia uzuri wa nchi na vivutio tulivyonavyo duniani. Na kwa kiasi kikubwa ulizaa matunda kwani wengi zaidi waliendelea kumiminika. 


Mbali na watu hao mashuhuri pia viongozi mbalimbali wa kiserikali kutembelea kwenye vivutio vya kitalii nchini kulileta hamasa kwa wananchi pia. Mwezi Oktoba, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu alipata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Bonde la Ngorongoro ambapo aliwahimiza watanzania kuendeleza juhudi za kuhifadhi na kutunza mazingira ya eneo hilo ili kuendelea kunufaisha kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. 


Lakini katika mwaka huo pia tulishuhudia mabadiliko kwenye sekta ya utalii ambapo Mh. Dkt. Hamisi Kigwangala aliteuliwa na Mh. Rais John Magufuli kuwa Waziri wa Utalii na Maliasili ambapo kupitia uongozi wake mpya tunaona mabadiliko na jitihada za dhati katika kuendeleza sekta hii ambayo ina mchango mkubwa katika pato la ndani la taifa na ajira. 


Kwa upande wa miundombinu, serikali kwa kiasi kikubwa imeendelea kuimarisha sekta ya mawasiliano kama vile barabara, reli, maji na anga ambapo imefanya uwekezaji mkubwa. Sehemu nyingi nchini zimekuwa zinafikika kwa urahisi kutokana na maboresho ya barabara huku uwekezaji mkubwa ukiwekwa katika ujenzi wa reli na kuzifufua za zamani. 



Yapo mengi ya kuvuna kutoka kwenye sekta ya utalii kama vile ajira na fedha ambazo zinasaidia kukuza pato la taifa. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Benki ya Taifa (BoT), mapato ya nje yaliyotokana na sekta ya usafiri, hususani sekta ya utalii, yameongezeka kwa zaidi ya ilivyokadiriwa na kufikia shilingi bilioni 128.8. Mapato hayo yamekuwa na kufikia Dola za Kimarekani bilioni 2,156.9 katika mwaka ulioshia mwezi Novemba 2017, kutoka Dola za Kimarekani 2,101.2 mnamo mwezi Novemba mwaka 2016, ambapo imechangiwa na kuongezeka kuja kwa watalii.