WATUHUMIWA 28 wanaokabiliwa na kesi ulipuaji mabomu katika sehemu mbalimbali Jijini Arusha na nje, wamefanya vituko vya mwaka katika Mahakama ya Mkoa wa Arusha.
Watu hao walivua nguo zao zote na kubaki uchi wa mnyama baada tu ya kufikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Arusha, kwa kile walichodai kushinikiza kusikilizwa kwa kesi yao.
Watuhumiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza kwa makundi tofauti tofauti kuanzia Julai 8 mwaka 2014 kwa tuhuma za ulipuaji wa mabomu kanisani, kumbi za starehe, migahawa na baadhi ya waamini wa dini ya Kiislamu kumwagiwa kitu kinachosemekana ni tindikali, hatua iliyoleta taharuki kali kipindi hicho katika Jiji la Arusha na viunga vyake.
hivyo, malalamiko ya watuhumiwa hao kutaka kesi hiyo ianze kusikilizwa kwa kuwa wamekaa katika gereza la Kisongo kwa muda mrefu, sio ya kwanza kwani walishawahi kufanya mgomo wa kutoshuka katika basi la magereza, kushinikiza kesi hiyo ianze kusikilizwa. Lakini, walijibiwa kuwa kesi yao inafanyiwa upelelezi ndani ya nchi na nje ya nchi, hivyo waliombwa kuwa na subira.
Watuhumiwa hao walifanya kituko hicho jana, mara baada ya kuwasili mahakamani hapo majira ya saa 2.45 asubuhi wakati askari magereza walipowaamuru kushuka ndani ya basi la Magereza kwa ajili ya kupelekwa mahabusu ndogo ya mahakama hiyo, kabla ya kuingia mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi zao mbalimbali zinazowakabili.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida wakati mahabusu hao wanashuka, askari Magereza hao walishangaa kuwaona 19 kati yao wakishuka uchi wa mnyama, hali iliyozua tafrani mahakamani hapo, ambapo watu mbalimbali wakiwemo mawakili, wananchi waliokuwa wamekuja kusikiliza kesi nyingine na watumishi wa mahakama hiyo, walipigwa na butwaa na hatua hiyo ya watuhumiwa kuvua nguo.
Wakati wanashuka ndani ya basi hilo huku wakiwa uchi, walisikika wakisema kuwa wamechoshwa na kitendo cha mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Arusha, kuahirisha kesi zao bila kusikilizwa kwa muda mrefu sana. Askari Magereza waliokuwa wamefurika mahakamani hapo na kuimarisha ulinzi kila kona, walipata wakati mgumu wa kuwasihi mahubusu hao waliokuwa na jazba kuvaa nguo. Mahabusu hao walikataa katakata na kudai kuwa watavaa nguo endapo wapata hatma ya kesi zao.
“Mawakili wa serikali kila siku wanakuja mahakamani hapa na kuieleza mahakama kuwa upelelezi haujakamilika, siku nyingine wanakuwa na sababu mbalimbali, sisi siyo watoto, tunataka kujua hatma yetu,” walidai. Baada ya kuingizwa rumande ya mahakama hiyo kwa muda, walifunguliwa mlango kwa ajili ya kupelekwa kizimbani, ambapo tisa ambao hawakuvua nguo awali, walikubali kuingia mahakamani.
Wakiwa mbele ya Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda, Wakili wa Serikali Agustino Kombe aliieleza mahakama kuwa upelelezi haujakamilika, hali iliyowafanya watuhumiwa hao, pia kuvua nguo mbele ya hakimu. Licha ya kuvua nguo, 19 kati yao waligoma kupanda kizimbani na kubaki rumande ya mahakama hiyo. Akizungumzia sakata hilo, Wakili Mfawidhi wa Serikali Mkoa wa Arusha, Maternus Marandu alisema kitendo kilichofanywa na mahabusu hao ni cha kihuni na utovu mkubwa wa nidhamu.
“Watuhumiwa hao wanatakiwa kutambua kuwa upelelezi ni jambo mtambuka, linalofanyiwa kazi na vyombo mbalimbali, siyo polisi peke yake, upelelezi huu unafanyika ndani na nje ya nchi na uhalifu unaodaiwa kufanywa ni mbaya sana,” alisema. Chanzo cha habari ambacho hakikutaka jina lake liandikwe gazetini, kilisema hizo ni mbinu chafu za kihuni, zilizopangwa na mahabusu hao kuvua nguo na kufanya vurugu ili askari waanze kujibu mapigo, wapate mwanya kutoroka.
“Mpango wao wa kuvua nguo ulikuwa ni mkakati wao wa kufanikisha kutoroka lakini tuliushtukia mapema sana, walitaka wavue nguo, wafanye vurugu, askari wajibu mapigo ili wapate mwanya wa kutoroka lakini hawajafanikiwa,” kilidai chanzo hicho.
Alipoulizwa kwa njia ya simu ya kiganjani, Kaimu Mfawidhi wa Mahahakama ya Wilaya ya Arusha/Arumeru, Jasmini Abdul alisema kuwa hakuwa na taarifa ya tukio hilo, kwa kuwa alikuwa akisikiliza kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, wakati tukio hilo lilifanyika katika Mahakama ya Mkoa iliyopo eneo la Uzunguni. Hakimu huyo alisema kuwa atafuatilia tukio hilo na kulitolea maelezo, baada kujua malalamiko yao watuhumiwa hao atakapofika eneo la tukio. Alimwomba mwandishi wa gazeti hili kuwa na subira. Alipotafutwa baadae, hakupokea tena simu yake ya kiganjani.
|
0 Comments