Wawekezaji katika sekta ya madini nchini Tanzania wanakabiliwa na sura mpya ya uwekezaji baada ya serikali kutunga kanuni mpya zitakazoongoza utekelezaji wa sheria mpya za madini nchini humo.
Mwaka jana, Tanzania ilipitisha sheria zilizoonekana kudhibiti vikali utendaji wa wawekezaji huku serikali ikitarajia kuvuna faida ya kutosha kutoka katika rasilimali kubwa ya madini iliyopo nchini.
Mathalani, sheria hizo zinatoa fursa kwa serikali kupitia upya mikataba yote ya madini na kutilia mkazo kwa kampuni shughuli za uchakataji madini kufanyika nchini. Sheria hizi pia zimebainisha wazi kwamba rasilimali madini ni mali ya taifa, kinyume na ilivyokuwa hapo awali ambapo hakuna sheria iliyokuwa imeweka wazi umiliki wa madini kwa taifa.
Pamoja na mambo mengine, kanuni hizi mpya ambazo kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Madini zimeanza kufanya kazi tangu mwezi uliopita, zinatoa kipaumbele si tu kwa taasisi za fedha na huduma za kisheria za Kitanzania lakini pia ajira kwa Watanzania.
Kuhusiana na huduma za kifedha, kanuni mpya zinataka makampuni ya madini kufungua akaunti na kuweka fedha zao katika benki za wazawa.
"Benki ya wazawa ni ile inayomilikuwa na wazawa kwa asilimia 100 ama ile ambayo Watanzania wanamiliki hisa nyingi zaidi", inafafanua sehemu ya kanuni hizo
Hii inaziengua benki kadhaa za kigeni kufanya biashara katika sekta ya madini. Baadhi ya benki za kigeni zinazofanya kazi nchini ni pamoja na Stanbic, Barclays, Standard Chartered na ile ya Afrika Kusini ya First National Bank (FNB)
Kanuni zinataka pia utoaji wa leseni za uchimbaji madini utoe kipaumbele kwa kampuni za kizawa kampuni zitakazoshindwa kutekeleza kanuni hizi zitatozwa faini ya hadi dola milioni 5 za kimarekani ($5 Milioni).
Kuna sheria zipi hadi sasa hivi?
Mwaka 2017, bunge nchini Tanzania ilipitisha sheria mbili muhimu za uchimbaji madini ambazo zina lengo la kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya madini.
Sheria hizo mbili zilifuatia mzozo wa miezi miwili kati ya serikali na kampuni ya uchimbaji madini ya Uingereza ya Acacia, kufuatia madai kuwa kampuni hiyo imekuwa ikikosa kulipa kodi.
Kupitia sheria hizo serikali inamatumaini kuwa wananchi watanufaika kutokana na mali asili ya nchi hiyo.
Moja ya sheria hizo inasema kuwa watu nchini Tanzania watakuwa na uhuru wa kudumu kwa mali yao ya asili na serikali kwa niaba ya watu itasimamia mali hiyo.
Hadi kupitishwa kwa sheria hio, sheria haikuweza kueleza wazi ni nani ana uhuru wa kusimamia mali asili ya nchi ya Tanzania.
0 Comments