Akwilina Akwilini
Makabiliano kati ya jeshi la polisi na wafuasi wa chama cha Chadema nchini Tanzania yalisababisha kifo cha mwanafunzi mmoja wa shule .
Mwanafunzi huyo wa Chuo cha usafirishaji Tanzania NIT ambaye jina lake na picha zilisambazwa katika mitando ya kijamii alipigwa risasi alipokuwa ndani ya basi siku ya Ijumaa, siku moja kabla ya uchaguzi mdogo wa eneo bunge la kinondoni.
Walioshuhudia wanasema kuwa maafisa wa polisi walitumia vitoa machozi na risasi katika harakati za kuwatawanya mamia ya wafuasi wa chama cha Chadema waliokuwa wakiandamana hadi afisi za tume ya uchaguzi.
Baadhi ya wanachama wa chama hicho walikamatwa.
Akizungumza na BBC mkuu wa Chuo hicho Prof Zacharia Mganilwa alithibitisha kuwa mwanafunzi wao wa shahada ya Manunuzi na Ugavi Akwilina Akwilini alifariki dunia siku ya Ijumaa.
Amesema kuwa mwili wa msichana huyo ulikuwa na jeraha la risasi kichwani.Kwa mujibu wa uongozi wa chuo hicho, mwanafunzi huyo alikuwa safarini kulekea Bagamoyo kupeleka fomu za kuomba nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo mjini Bagamoyo
Aidha kamanda wa polisi mjini Dar es Salaam Lazaro Mambosasa alikiri kwamba mtu mmoja alipigwa risasi na kufariki wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa chama cha Chadema waliokuwa wakiandamana.
Ghasia hizo zilianza baada ya wafuasi wa Chadema kuanza kuandamana wakielekea katika afisi hizo wakitaka wanachama wao kupewa vibali vya kuwa waangalizi katika uchaguzi huo.
|
0 Comments