MABALOZI wapya wa Tanzania katika nchi za Sweden na Nigeria, Dk Wilbrod Slaa na Muhidin Mboweto, wamemuahidi Rais John Magufuli kwamba watafanya kazi zao katika vituo hivyo kwa bidii, weledi na uadilifu huku wakitanguliza mbele uzalendo kwa maslahi ya Taifa.

Dk Slaa na Mboweto waliapishwa jana Ikulu jijini Dar es Salaam na Rais Magufuli, baada ya kuwateua kuiwakilisha Tanzania katika nchi hizo kuwa mabalozi. Novemba 23, mwaka jana, Rais Magufuli alimteua Dk Slaa kuwa Balozi na kueleza kuwa atampangia kituo cha kazi baadaye.
Mboweto aliteuliwa kuwa Balozi, Januari 19. Dk Slaa ni mwanasiasa maarufu nchini aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokarasia na Maendeleo (Chadema) hadi alipoachia ngazi Agosti 2015, akitofautiana na wenzake katika uteuzi wa mgombea urais. Akizungumza baada ya kuapishwa, Dk Slaa alimshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi wake huo, akisema ameona kuwa kwa vigezo vyake anastahili kazi hiyo, hivyo kumuahidi kuwa hatamuangusha.
Alieleza kuwa atazingatia vipengele vyote vya kiapo, alichokula muda mfupi baada ya kuapishwa, kwa maslahi mapana ya Taifa la Tanzania kwani kulitumikia taifa ni heshima kubwa. “Mimi huwa sipendi kutoa ahadi, lakini naahidi nitaitumikia nafasi hii kwa moyo wangu wote, uwezo wangu, akili zangu na nguvu zangu zote kwa ajili ya Taifa langu hasa wakati huu tunapozungumzia Tanzania ya viwanda tukiwa na nia ya kuwa taifa lenye uchumi wa kati,” alieleza Dk Slaa.
Alisema maendeleo ni safari, na kwamba kwa muda mrefu tangu akiwa bungeni, msisitizo umekuwa ni kuwa na diplomasia ya kiuchumi, hivyo anamshukuru Rais Magufuli kwa kuliona hilo na kulitilia mkazo, na kwamba na yeye ataenda kulisimamia kikamilifu katika kituo chake cha kazi Sweden. Kwa upande wake, Balozi Mboweto licha ya kumshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi huo, aliahidi kwenda kufanya kazi kwa bidii, weledi na kuzingatia maadili, huku akitanguliza uzalendo kwa Tanzania.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Suzan Kolimba aliahidi kuwa wizara itawapa ushirikiano mabalozi hao huku akiwataka wakafanye kazi kwa weledi wakitanguliza mbele uzalendo kwa Taifa, na kusisitiza diplomasia ya uchumi katika vituo vyao vya kazi. Kwa mujibu wa taarifa ya jana asubuhi iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, uteuzi wa mabalozi hao kuiwakilisha Tanzania katika nchi walizopangiwa, umeanza Februari 15, 2018.