WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuisaidia Tanzania kutokana na mchango mkubwa wa kuwahudumia wakimbizi, ambao imekuwa ikiutoa kabla na baada ya uhuru, licha ya uchumi mdogo ilionao.

Waziri Mahiga alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam katika kikao cha Baraza la Wakimbizi Duniani (WRF), kinachofanyika kwa siku mbili kuanzia jana.
Mahiga alieleza kuwa Tanzania ilipokea wakimbizi kutoka Poland wakati wa Vita ya Pili ya Dunia na mwaka 1959 ilipokea wakimbizi kutoka nchi ya Rwanda.
Aidha, baada ya Uhuru, Tanzania imekuwa ikipokea wakimbizi mara kwa mara na wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, Tanzania ilipokea wakimbizi wengi zaidi duniani.
Alisema athari zinazotokana na kupokea wakimbizi wengi ni nyingi na kubwa hivyo, ni jukumu la jumuiya ya kimataifa kuzisaidia nchi zenye wakimbizi wengi, hususan zile zenya uchumi mdogo.
Katika kikao hicho, Waziri Mahiga alitoa ufafanuzi kuhusu msimamo wa Serikali ya Tanzania kujitoa katika Mpango wa Kutafuta Suluhu ya Kudumu ya Tatizo la Wakimbizi Duniani (CRRF).
Alisema katika Mpango huo wa CRRF, Serikali imesikitishwa na mapendekezo ya mpango huo ya kuitaka Tanzania ikope fedha kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi na kugharamia ukarabati wa miundombinu iliyoharibika.
Halikadhalika, CRRF inapendekeza kuwepo na utaratibu wa kuwapa uraia, ajira na ardhi wakimbizi wanaoingia nchini ili waweze kuwa huru na kujitegemea.
Alibainisha kuwa serikali ilishatoa uraia kwa wakimbizi zaidi ya 150,000. Jumuiya ya kimataifa iliahidi kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia makazi na huduma nyingine kwa wakimbizi hao. Hata hivyo, jumuiya ya kimataifa haijatekeleza ahadi hiyo, badala yake inaitaka Serikali ichukue mkopo wenye riba kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi.
“Misitu, ardhi, mazingira na miundombinu mingine inaharibika kwa sababu ya wakimbizi, halafu tuchukue mkopo na kulipa deni kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi, nadhani si utaratibu mzuri,” alisisitiza Dk Mahiga.
Dk Mahiga alieleza kuwa amewasilisha ujumbe wa serikali kwenye baraza hilo ili lifikishe kilio cha Tanzania katika Jumuiya ya Kimataifa kwa matumaini kuwa wao wanasikilizwa zaidi.
Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alitoa maelezo kuhusu dhamira ya kuanzishwa kwa WRC.
Alisema WRC ilianzishwa mwaka 2017 kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Canada na taasisi isiyo ya kiserikali ya nchi hiyo.
Lengo la chombo hicho ni kuangalia sababu zinazofanya wakimbizi kuongezeka, matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na kutoa maoni ya namna ya kutatua tatizo la wakimbizi duniani.