live it love it
DAR ES SALAAM, FEBRUARY 2018. Milvik Tanzania na Tigo wamechaguliwa katika tuzo za Uvumbuzi Bora wa simu za mkononi katika soko linalochipukia katika kundi la Ubora kwa jamii (Social good) katika Tuzo za Simu za Mkononi za GSMA. Tuzo hizi za heshima zinalenga kutambua na kusherehekea mchango uliotolewa katika sekta ya simu za mkononi inayoendelea  kubadilika duniani kote. 
Tuzo za Uvumbuzi Bora wa simu za mkononi katika soko linalochipukia zinatambua uvumbuzi halisi katika jitihada za simu za mkononi ambazo zinalenga kutambua mchango unaotolewa na makampuni katika ushirikishaji, upatikanaji na uhai wa masoko yanayochipukia. Uteuzi huo unalenga kutambua juhudi za Milvik na Tigo kwa jamii kwa kuwapatia wateja ambao mwanzo walikuwa wamesahaulika katika huduma za bima ya afya kwa gharama nafuu.
Milvik imeleta gharama ndogo za upatikanaji wa huduma ya bima Afrika kwa masoko yanayochipukia (3% tu) kwa kuunganisha pamoja nguvu ya teknolojia ya simu za mkononi na makampuni ya simu kufungua upatikanaji mpya wa huduma nafuu za mawasiliano, na kuunganisha jamii za pembezoni zilizokuwa zimesahaulika katika huduma muhimu za bima kwa lengo la kuleta ushirikishwaji jumuishi wa kifedha. 
Milvik na Tigo wameanzisha mfumo wa kwanza wa kidigitali wa bima katika simu za mkononi kwa kuunganisha mfumo wake wa bima katika simu za mkononi na miundombinu ya teknolojia ya makampuni ya simu, jambo ambalo linawawezesha wateja  kujiunga na kulipia bima kupitia simu zao za mkononi.
Nchini Tanzania, Milvik inashirikiana na Tigo kuleta huduma za bei nafuu za bima kwa wateja wa Tigo ambapo wataweza kulipia bima zao kwa kutumia fedha zilizoko katika simu.  Ushirika huu wa Tigo/Milvik kwa sasa unatoa moja kati ya huduma kubwa zaidi ya bima ya kulipia kupitia simu za mkononi duniani. 
Hussein Sayed, Afisa Mkuu wa Huduma za Kifedha wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo, amesema: “ninafuraha kwamba kazi ambayo Tigo na Milvik wamefanya katika kuleta ushirikishwaji wa kifedha kupitia uvumbuzi huu unaanza kutambulika. Kwa kuwezesha upatikanaji wa bima kupitia simu za mkononi, wateja ambao kwa kawaida wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kupata huduma za kifedha kupitia taasisi zingine, kwa sasa wataweza kupata ulinzi wa kifedha, wao na familia zao. Tunajisikia furaha kushirikiana na Milvik kutoa bidhaa zenye thamani kubwa za bima kwa wateja wetu pamoja na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.”
Tom Chaplin, Meneja wa Milvik Tanzania, kwa upande wake alisema: “Kupitia mfumo wetu wa bima kwa simu za mkononi na ushirika wetu na Tigo, tumeweza kusambaza huduma rahisi ya bima na yenye bei nafuu kwa watu wengi na kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za msingi za kifedha. Kadri ambavyo huduma za simu zinavyozidi kujipenyeza katika masoko yanayochipukia, tunaona fursa nyingi katika kushirikiana na makampuni ya simu na kuwapatia watu zana za kifedha wanazohitaji kuhakikisha mafanikio yajayo ya kiuchumi na familia zao.”
Mshindi wa Tuzo hizo atatangazwa katika Kongamano la Simu za Mkononi Duniani (Mobile World Congress) Barcelona, litakalofanyika kuanzia tarehe 26 Februari mpaka tarehe 1 Machi mwaka huu.