Takriban watu saba wameuawa katika vita ambavyo vilizuka baada ya msichana wa dini ya Kikristo kubadili dini na kuwa Mwislamu Kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Vita hivyo vilivyozuka katika jimbo la Kaduna viliwaacha watu 15 wakiwa na majeraha baada ya nyumba kuchomwa moto.
Shahidi mmoja aliambia BBC kwamba tatizo lilianza baada ya msichana huyo wa Kikristo kutoka Gwari kubadili dini na kuwa Muislamu kutokana na ushawishi wa mpenzi wake.
Shahidi anasema kuwa tatizo hilo liliwachochea vijana wa Kikristo .
Ripoti nyengine zinasema kuwa wasiwasi kati ya wafuasi wa dini hizo mbili ulikuwa tangu awali.
Hata hivyo kamanda wa polisi wa Kaduna Muktar Aliyu aliambia BBC kwamba huku wakifanikiwa kuwakamata watu 10 wanaohusianana na kisa hicho, maafisa bado wanachunguza sababu ya vita hivyo.
''Hatuwezi kuthibitisha kwamba vita vilizuka kwa sababu kuna mtu alibadilisha dini na kuwa Mwislamu ama dini nyengine yoyote ile'', alisema.
''Watu wana haki ya kubadili dini na kuingia dini nyingine yoyote ile, hatua hiyo haifai kuchochea vita''.
Anasema kuwa hatua zimechukuliwa kuzuia vita hivyo kuenea kutoka Kasuwan Magani eneo ambalo ni kilomita 36 kutoka mji mkuu, hadi maeneo mengine.
|
0 Comments