Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amewapokea wasichana 106 na mvulana mmoja jijini Abuja.Wasichana waliwasili mapema kwenye makazi ya Rais wakionekana wenye afya njema, isipokuwa wanne ambao wanaelezwa kuwa walivunjika miguu.
Wasichana walisafirishwa kwa ndege mpaka mjini Abuja siku ya Jumatano ambapo walitakiwa kwenda kufanya uchunguzi wa kitabibu na kiusalama baada ya kukabidhiwa kwa mamlaka za kiraia.
Buhari amewataka wasichana waendelee kutimiza ndoto zao bila kuogopa machafuko, amevitaka vyombo vya ulinzi kuhakikisha usalama unakuwepo kwenye shule zote zilizo hatarini kushambuliwa na kuonya kuwa iwapo tukio hilo litatokea tena hatalichukuliwa kirahisi.
Buhari amewataka wazazi ambao bado watoto wao wanashikiliwa kutokata tamaa wakati serikali yake inafanya jitihada kuwanasua.
Wasichana wanatarajiwa kupewa ushauri nasaha kabla ya kukabidhiwa kwa wazazi wao.
Haijulikani kama kurejea kwao kwenye maisha ya kawaida ni suala la uchaguzi wakati huu ambao mustakabali wa elimu yao haujulikani, iliripotiwa kuwa wakati mabinti hao walipokuwa wakirejeshwa, wanamgambo walitoa tahadhari kuwa wasirejee tena shuleni.
Wakati hayo yakijiri Serikali ya Nigeria imesema haitapunguza jitihada zake za kumkomboa msichana mmoja aliyebaki mikononi mwa Boko Haram baada ya kutekwa mjini Daptchi mwezi uliopita.
Msichana huyo ni miongoni mwa wasichana 110 waliochukuliwa wakiwa shuleni, wanamgambo walipovamia mji tarehe 19 mwezi Februari.
Wengi wao waliachiwa siku ya Jumatano isipokuwa msichana mmoja, Mkristo ambaye alikataa kubadili dini kuwa muislamu, anashikiliwa bado .
Rais alisema msichana huyo hatatelekezwa.
''Rais Muhammadu Buhari amejitoa kuhakikisha msichana wa Dapchi aliyebaki anakuwa huru''. Ilieleza taarifa ya serikali.
''Serikali ya Buhari haitaacha jitihada za kumnasua binti na kumrejesha kwa wazazi wake.Msichana huyu hatatelekezwa''.
Kati ya waliotekwa, wasichana 104 waliachiwa siku ya Jumatano na watano wanaripotiwa kupoteza maisha wakiwa mateka.
Watu wengine wawili , mvulana na msichana mwingine kutoka mji wa Dapchi waliachiwa huru wakati huo huo, serikali imesema.
Serikali imekana madai kuwa Boko Haram walilipwa pesa kuwakomboa wasichana, au kubadilishana na mfungwa.
Waziri wa Habari Lai Mohammad ameiambia BBC kuwa kurudi kwa wasichana ni sehemu ya mazungumzo yanayoendelea kuhusu msamaha na kusitisha mapigano.
''hatukulipa pesa yoyote kwa ajili ya wasichana.Tulijadiliana mpango wa kumaliza mapigano tukiahidi kuwasamehe''.Alieleza.
''Kama wao(Boko Haram) wataweka silaha zao chini na kuukana uasi, sisi tutawapa njia huru kabisa kurejea kwenye jamii''.Alisema bwana Mohammad.
Amesema serikali ilikuwa imerudishwa nyuma na kitendo cha utekaji wa wasichana na kuharibu mazungumzo .
Wakati huohuo, Baba wa msichana mmoja kati ya waliotekwa ameeleza uchungu alioupata kutokana na kumpoteza binti yake tena baada ya kwenda kukutana na Rais muda mfupi baada ya kuachiwa.
Ameiambia BBC aliweza kumuona binti yake hospitali tu,tena kwa dakika chache.
Utawala wa Buhari umekuwa kwenye shinikizo kukomesha vitendo vya utekaji nyara, uliorudisha kumbukumbu ya mwaka 2014 , wasichana 276 mjini Chibok walipotekwa
Rais wa zamani wa Nigeria , Goodluck Jonathan alikosoa namna ambavyo rais Buhari anavyoshughulikia utekaji nyara wa Chibok, takriban umbali wa kilometa 275 kusini mashariki mwa mji wa Daptchi.
Zaidi ya nusu ya waliotekwa Chibok wamerejea lakini 100 bado hawajulikani walipo.
Shirika la waangalizi wa haki za binaadam, Amnesty International limekosoa namna serikali inavyoshughulikia suala la utekaji nyara uliofanyika Daptchi, likisema serikali ilipuuza maonyo mbalimbali kuhusu nyendo za wapiganaji wa Boko Haram kabla ya kuwateka nyara wasichana.
Jeshi la Nigeria limesema madai ya Amnesty International ni uongo mtupu.Shirika la habari la Ufaransa AFP limeripoti.
0 Comments