MENEJA wa Shirika la Kikristo lisilokuwa la kiserikali la World Vision Kanda ya Kati, Faraja Kulanga amesema Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa vinara wa mimba za utotoni.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za kupinga mimba za utotoni wilayani Chemba, Kulanga alisema, Dodoma ni ya tatu katika mikoa ambayo ina idadi kubwa ya mimba na ndoa za utotoni.
Ameyasema katika utafiti uliofanyika na Shirika la Afya la Utafiti, ulionesha kwamba asilimia 53 ya wanawake waliohojiwa walisema walipata ujauzito wakiwa na umri chini ya miaka 18.
Amesema, katika shule za msingi watatengeneza kamati za watoto ambazo watazijengea utashi wa namna gani wanaweza kujikinga na majanga hayo.
Akifungua kampeni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga, amesema anajisikia aibu kwa wilaya yake kuwa miongoni mwa wilaya vinara katika udhalilishaji watoto wa kike ikiwemo mimba na ndoa za utotoni.
Odunga alisema: “Hatutavumilia kuona mkazi yeyote wa wilaya ambaye kwa namna moja amechangia kufanikisha au kufanya jambo hilo la aibu kwa wilaya hii.
"Dodoma ipo kati ya mikoa 13 inayofanya vibaya katika eneo hili. Katika wilaya zinazofanya vibaya nasikitika pia Chemba ni wilaya mojawapo. Naona aibu sana kusimama kama Mkuu wa Wilaya inayodhalilisha watoto," alisema.
0 Comments