Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Kenyatta nchini Kenya ametumwa kwenye likizo ya lazima baada ya mgonjwa ambaye hakufaa kufanyiwa upasuaji wa ubongo kufanyiwa upasuaji huo katika hospitali hiyo.
Hatua ya kumtuma Lilly Koros kwenye likizo ya lazima imetangazwa na Waziri wa afya Sicily Kariuki ambaye amesema hatua hiyo inakusudiwa "kupisha uchunguzi".

Kisa hicho ambacho kimewashangaza wengi kilitokea katika hospitali hiyo wiki iliyopita na leo ilikuwa tarehe ya mwisho kwa maafisa wa matibabu ambao walihusika kueleza ilikuwaje hadi kosa hilo likatokea.
Taarifa ya Bi Koros iliyotolewa Alhamisi ilisema maafisa wanne wa matibabu walikuwa wamesimamishwa kazi, akiwemo msimamisi wa sajili ya watu wanaofanyiwa upasuaji wa ubongo.
Wengine ni mwuguzi aliyekuwa akisimamia wadi, mwuguzi wa kuwapokea wagonjwa kwenye chumba cha kufanyiwa upasuaji na afisa wa kuwatia ganzi wagonjwa.
Bi Koros alisema kupitia taarifa kwamba kosa hilo lilitokea pale mkanganyiko ulipotokea kuhusu wagonjwa wawili waliokuwa hawajitambui.
Mmoja kati yao ndiye alihitaji upasuaji wa kichwa ili kuondoa damu iliyokuwa imeganda kwenye ubongo wake.
Huyo mwingine alikuwa amefurwa kwenye kichwa lakini alihitaji matibabu ambayo hayakushirikisha upasuaji.
Lakini asiyehitaji upasuaji ndiye aliyeishia kufanyiwa upasuaji. Madaktari waligundua kosa hilo saa chache baada yao kuanza upasuaji walipogundua kwamba hawakuweza kuiona damu iliyoganda kwenye ubongo wa mgonjwa waliokuwa wanamfanyia upasuaji.
Bi Koros ameomba radhi na kusema "tunafurahi kuwatangazia umma kwamba mgonjwa huyo sasa ametibiwa na anaenedelea vizuri kupata nafuu".

Wakenya walivyopokea habari hizo

Wakenya wameeleza hisia zao katika mitandao ya kijamii ya Twitter.
"Jinsi mambo yanavyoharibika kwa haraka Kenya National hospital"
"Ukienda na kitambi kwenye hospitali ya taifa ya Kenyatta, unaweza ukute unapelekwa wadi ya wajawazito"
Wadi Hospitali ya KenyattaHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Hili sio sakata la kwanza kukumba hospitali hiyo, mwezi wa kwanza mwaka huu, waziri wa afya nchini Kenya Dkt Cleopha Mailu aliamrisha uchunguzi ufanyike baada ya wanawake waliojifungua kudai kwamba wanadhalilishwa kingono.
Taarifa zilizoenezwa kwenye mitandao zilidai kina mama waliojifungua wamekuwa wanashambuliwa na baadhi ya wafanyikazi wakati wakienda kwenye chumba cha watoto wachanga kuwanyonyesha watoto wao.
Tukio hilo liliibua maandamano na wanaharakati na wanawake walikasirishwa na usalama duni na utendaji kazi wa hospitali hiyo.
Kisa karibu sawa Tanzania
Kwa upande wa Tanzania, kisa kama hiki kiliwahi kutokea mwaka 2007.
Tarehe 8 Novemba, madaktari wawili wa upasuaji wa ubongo katika hospitali ya rufaa ya Muhimbili walimpasua kichwa Emmanuel Didas kutoa uvimbe ambao haukuwepo.
Wakati mgonjwa Emmanuel Mgaya, aliyekuwa na uvimbe huo alipasuliwa goti.
Madaktari hao walichukuliwa hatua na kufutwa kazi na mamlaka ya hospitali.
Makosa Uingereza na India
Si Afrika pekee ambapo makosa kama hayo hufanyika. Kipindi cha BBC cha Victoria Derbyshire mwaka jana kilibaini kwamba makosa takriban 1,400 hufanyika kila wiki katika hospitali za kujifungulia kina mama nchini England kila wiki.
Mwishoni mwa mwaka jana nchini India, mtoto aliyekuwa amedaiwa kufariki baada ya kuzaliwa katika hospitali moja mji mkuu wa Delhi alibainika kuwa hai jamaa zake walipokuwa wanaelekea kumzika.