Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi
MAOFISA Habari, Uhusiano na Mawasiliano serikalini wametakiwa kujitambua na kufanya kazi kisasa, lengo likiwa ni kufanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi katika Mkutano wa Chama cha Maofisa Habari Serikalini (TAGCO) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC). Dk Abbasi alisema umefika wakati wa maofisa habari wa wizara, taasisi za serikali, mikoa, majiji na halmashauri kujitambua na kujithamini na kufanya kazi hiyo kwa kujiongeza ili kwenda sambamba na kasi ya teknolojia ya karne ya 21.

Alisema kila mmoja katika eneo lake la kazi anapaswa kujituma kwa lengo la kufanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa ili jamii ijue kuwa kazi aliyopewa haikuwa ya kubahatisha. Msemaji huyo wa serikali alitoa mfano alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO, vitendea kazi vilikuwa vichache lakini alipojitambua na kujiongeza sasa idara hiyo iko vizuri na ina vifaa vya kutosha na vya kisasa na kuwataka maofisa habari wa kila eneo kufanya hivyo.
Alisema baadhi ya wizara (bila kuzitaja) maofisa habari wake hawafanyi kazi ipasavyo na amekuwa akipigiwa simu na mawaziri wao juu ya hali hiyo hivyo alionya kuwa sasa hatavumilia hali hiyo ikijitokeza baada ya mkutano huo. “Nawaomba maofisa habari mjitambue na mjithamini katika utendaji kazi wa kila siku na muache kulalamika kuwa hamthaminiwi. “Jukumu lenu ni kufanya kazi iliyotukuka katika maeneo yenu ya kazi na kuacha tabia ya kusubiri kuandika taarifa kwa vyombo vya habari pindi mawaziri na viongozi wa maeneo yenu ya kazi wanapotaka kuzungumza,” alisema.
Aliwataka kutoa taarifa iliyo shiba ya maeneo yao ya kazi katika mitandao ya kijamii ili kupima kama kazi zao zinakubalika au hazikubaliki kwa vile ndio kipimo cha kazi zao kwa vile hivi sasa jamii kubwa ipo mitandaoni. Aliwataka maofisa hao pia kujenga utamaduni wa kujiwekea malengo akitolea mfano wa Rais John Magufuli aliyejiwekea malengo ya kununua ndege sita na kutekeleza malengo yake.
“MAELEZO tumejiwekea malengo yetu na tunayatekeleza, TSN (Shirika la Magazeti ya Serikali) nao wamejiwekea malengo na wamefanikiwa, kwa nini wewe uliyeko wizarani, taasisi ya serikali, mkoani, kwenye majiji au halmashauri ushindwe kufanya hivyo? Alihoji. Mkutano huo wa siku tano uliohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 300 unatarajiwa kumalizika kesho na baada ya mada mbalimbali za ufanisi katika kazi kujadiliwa na baadhi ya magwiji wa habari nchini na wadau wa habari, lengo likiwa ni kuboresha utendaji kazi katika karne hii ya 21 ya teknolojia ya kisasa.