WIZARA ya Mambo na Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imethibitisha kifo cha mwanafunzi Mtanzania aliyekuwa akisoma nchini Afrika Kusini.
Akizungumza na gazeti hili, Msemaji wa Wizara hiyo, Mindi Kasiga alifafanua kuwa kwa sasa wizara imewasiliana na Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ili kubaini undani wa suala hilo.

Alisema wizara bado haina taarifa za kina kuhusiana na suala hilo na kuwa inafuatilia kujua chuo alichokuwa akisoma, siku ya tukio hilo na masuala yote muhimu kuhusiana na kifo hicho.
Jana kulikuwa na taarifa iliyokuwa ikizunguka kwenye mitandao ya kijamii ikielezea kuwa kuna Mtanzania ameuawa kikatili nchini Afrika Kusini. Taarifa hizo zilidai kuwa mwanafunzi aliyejulikana kwa jina la Baraka Nafari aliyekuwa akichukua Shahada ya Uzamivu (PHD) katika Chuo Kikuu cha Johannesburg (UJ) aliuawa mapema Ijumaa Februari 23, mwaka huu kwa kugongwa na gari mara mbili na kubamizwa kwenye ukuta na baadaye kushambuliwa kwa visu.
Ziliendelea kudai kuwa kamera za usalama za CCTV za chuo hicho zilionesha Baraka na mwanafunzi mwenzake wakikimbia kujiokoa wakati wanaume wawili kwenye teksi wakiwaandama. Kwa mujibu wa taarifa hizo kamera hiyo iliendelea kumuonesha dereva wa teksi akimgonga kwa makusudi mwanafunzi huyo kwenye uzio wa makazi ya chuo hicho yaliyoko Auckland Park na kumuua.
Taarifa hizo ziliendelea kusema kuwa dereva wa gari hilo alikamatwa na polisi kwa kuendesha bila leseni, lakini baadaye aliachiwa huru bila kufunguliwa mashtaka yoyote. Kwa mujibu wa taarifa hizo, zinazoonekana kuandikwa na wafanyakazi na wanafunzi wa chuo hicho wakitaka polisi na uongozi wa chuo kuchukua hatua dhidi ya mauaji ya mwanafunzi huyo waliomuelezea kuwa alikuwa akipendwa na wafanyakazi na marafiki wa Chuo hicho na kuwa hawataacha maswali kuhusu mazingira ya kuuawa kwake bila kupata majibu.