TUME ya Taifa ya Uchaguzi (MEC) imejibu malalamiko yaliyotolewa na Mwenyekiti wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kwa kuainisha majibu ya hoja zote zilizotolewa dhidi yake.

Majibu hayo ya NEC kwa Mbowe yalitolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima. Aidha Nec imesema ipo tayari kumpa elimu ya mpiga kura Mbowe na wanachama wa Chadema ili kupanua uelewa wao kuhusiana na masuala ya sheria za uchaguzi. “Malalamiko yaliyotolewa na Mbowe yametusikitisha sana. Madai kwamba tume haikuwajibu malalamiko yao si kweli, ni upotoshaji wa hali ya juu ambao haupaswi kufanywa na kiongozi kama yeye. “Chadema walitaka wakati wa kampeni, Tume ifanye maamuzi kinyume cha maadili waliyoyasaini.
Wakati wa kampeni kuna kamati za maadili ngazi ya jimbo ambayo Mwenyekiti ni Msimamizi wa Uchaguzi na wajumbe ni kutoka vyama vyote vilivyosimamisha wagombea na ndio wanaofanya uamuzi. “Chadema waliwasilisha malalamiko kwa Tume badala ya kuwasilsiha malalamiko kwenye kamati hizo za maadili zinazosimamia malalamiko yote. Si sahihi kusema Tume hatukujibu malalamiko yao,” alisema Kailima. Majibu ya hoja za Chadema Akizungumzia namna NEC ilivyojibu hoja za Chadema, Kailima alisema hoja ya kwanza ilikuwa ni ombi la chama hicho kutaka kuapishwa mawakala wao mbadala asilimia 15.
“Tuliwajibu kwamba hakuna kifungu cha sheria kinachokipa fursa chama chochote cha siasa kuapishiwa mawakala mbadala asilimia 15. Kifungu 57 (3) kinafafanua vizuri namna ya mawakala wanavyotakiwa kuwepo na kuapishwa “Lakini pia hata kama kifungu hicho kingekuwa kinatoa fursa hiyo, Chadema walileta malalamiko yao Februari 15, 2018 wakati uteuzi wa mawakala ulikuwa Februari 10, 2018, hivyo hakukuwa na muda wa kuwaapisha mawakala wengine kwa mujibu wa sheria kwa kuwa hawakuwemo kwenye orodha.”
Alisema hoja ya pili ya Chadema ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni alikataa kuwapa mawakala barua na fomu za viapo. “Tulifanya hesabu tukaona kwamba msimamizi alitakiwa kusaini barua 22,000 na fomu za viapo 14,000. Tukasema kwamba kutakuwa na utaratibu wa mawakala kupewa fomu na viapo vyao kupitia kwa wawakilishi wao na walipewa kwa njia hiyo. Hili tuliwajibu hivyo katika barua yetu.”
Kuhusu hoja ya tatu, Kailima alisema mawakala wa Chadema waliambiwa kwenda na vitambulisho kwenye vituo vya kupigia kura na waliwajibu kwamba wakala wa chama cha siasa ni mpiga kura kama walivyo wapiga kura wengine. “Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia sheria ya uchaguzi kifungu namba 61 na namba 62 cha sheria za Serikali za mitaa, Tume ilitoa ridhaa kwa wapiga kura kutumia vitambulisho mbadala ili nao waweze kupiga kura ndiyo maana wakaelekezwa kwenda navyo.”
Hoja ya nne ilikuwa ni kwamba Msimamizi wa Uchaguzi Kinondoni, hajatoa maelekezo ya ni wapi pa kuhesabia kura na walijibiwa kwamba Tume ina barua kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi akiwajulisha vyama vya siasa kwamba sehemu ya kujumlishia kura itakuwa ni sehemu ya Biafra. “Kanuni inasema wangejulishwa eneo hilo la kujumlishia baada ya kura kupokelewa, lakini Msimamizi wa Uchaguzi alijiongeza akawajulisha mapema eneo la kujumlishia kura.
Hoja ya tano ilikuwa ni wasimamizi wa vituo hawakuteuliwa kwa utaratibu na majibu yalikuwa ni kwamba sheria ya uchaguzi imeweka utaratiibu wa namna wasimamizi hao wanavyopatikana. Lakini kanuni za uchaguzi wa Rais namba 15 na kanuni 11 za Serikali za Mitaa zinaeleza namna msimamizi wa kituo anavyopatikana. “Kanuni hiyo inasisitiza kuwa msimamizi wa uchaguzi atatoa tangazo. Kwa jimbo la Kinondoni, Msimamizi alitoa tangazo, watu waliomba, walifanya usahili na kabla ya uteuzi Mkurugenzi wa Uchaguzi alitoa matangazo ya majina katika mbao zote za kata 10 za Jimbo la Kinondoni.
“Msimamizi wa Uchaguzi aliwaandikia barua vyama vyote kama vina pingamizi vijitokeze. Kama kulikuwa na tatizo vyama vilikuwa na fursa ya kuweka pingamizi, lakini hawakufanya hivyo na Tume tuliwajibu hivyo. “Unaposema Tume haikuwajibu si kweli, labda Chadema waseme tuliwajibu nje ya matakwa yao waliyotaka na si kwa mujibu wa sheria. Hoja ya sita ilikuwa ni kwamba kuna wizi wa kura na majibu yalikuwa ni kwamba katika kituo cha kupigia kura kuna msimamizi wa kituo, msimamizi msaidizi na wakala wa chama cha siasa na kuna waandishi wa habari.
“Utaratibu ulikuwa wazi. Pia kuna utaratibu wa kisheria wa kuwasilisha malalamiko kama mtu haridhiki kabla, wakati na baada ya kupiga kura, wakati wa kuhesabu na baada ya kuhesabu kura. “Tunamsihi Mbowe na chama chake, wasome sheria za uchaguzi na kuzielewa. Tume iko tayari kumpa elimu ya mpiga kura kuzifahamu sheria hizi kwa mapana yake.
Pia tunamwomba kama hakuridhika na taratibu za uchaguzi, ana fursa ndani ya siku 30 za kuwasilisha malalamiko yake mahakamani ndicho chombo pekee cha kutoa haki. “Aende mahakamani kwa kutumia ushahidi ambao mawakala wake walijaza kwenye fomu namba 14 na 16 kwa sababu Tume ya Uchaguzi haina tena fursa ya kupokea malalamiko kisheria baada ya uchaguzi kupita,” alisema Kailima.