Zaidi ya simba 200 huuwawa kila mwaka nchini Tanzania na wafugaji waishio pembezoni mwa mbuga za wanyama na maeneo mengine ya uhifadhi.
Hiyo ni kwa mujibu wa mtafiti na mhifadhi kutoka Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori Tanzania.

Dkt Dennis Ikanda ameiambia BBC kwamba kufuatia idadi ndogo ya simba iliopo hivi sasa ulimwenguni kote, kuna haja ya hatua madhubuti kuchukuliwa kukomesha migogoro kati ya wafugaji na wanyamapori.
Ongezeko la idadi ya mifugo na uhaba wa maeneo ya kulishia mifugo inawasukumua wafugaji wengi kwenda kutafuta malisho karibu na mipaka ya maeneo ya uhifadhi.
Wafikapo huko, ndipo hukutana na simba na wanyamapori wengi ambao huwashambulia mifugo wao.
Hivyo, simba wanaposhambulia wanyama wao, wafugaji pia wanawaua simba.
Hata hivyo Dkt Ikanda anasema hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kwamba simba wako hatarini kutoweka siku za hivi karibuni.
"Tanzania ina idadi kubwa sana ya simba na hii ni kutokana na eneo kubwa lililotengwa kwa ajili ya uhifadhi wa simba na wanyama wengine." Dkt Ikanda ameiambia BBC.
"Tunakadiria kwamba idadi ya simba ni kati ya 16,000 na 17,000 ambao wapo maeneo ya uhifadhi ambayo yako mbali na maeneo ambayo wakulima huyafikia. Kwa hivyo, tutaendelea kuwa na simba mradi tu mipaka hii ya uhifadhi itatunzwa na kuheshimiwa."
Hata hivyo Dkt Ikanda amesema elimu zaidi ya uhifadhi inahitajika kwa jamii ziishizo pembezoni mwa maeneo ya uhifadhi juu ya umuhimu wa simba na wanyamapori kwa ujumla, ili wafahamu mchango wao katika pato la taifa.
Amesema pia kuna haja ya kuwasaidia wakulima kupata vyanzo vingine vya mapato ili wasiendelee kutegemea mifugo tu kukidhi mahitaji yao ya kiuchumi.
Mbuga ya Ruaha iliyopo kusini mwa Tanzania inaaminika kuhifadhi takribani asilimia 10 ya idadi ya simba iliyopo duniani kote.