Zaidi ya madaktari 500 katika hospitali kuu ya Kenyatta nchini Kenya wamesusia kazi wakitaka kurejeshwa kwa mwenzao aliyesimamishwa kazi baada ya kumfanyia kimakosa mgonjwa upasuaji wa kichwa.
Kadhalika wanadai marupurupu ambayo wanasema hawajalipwa.
Mwenyekiti wa Muungano wa Madaktari nchini, Samuel Oroko, amesema kumsimamisha kazi daktari huyo ilikuwa ni uamuzi ambao hauwezi kutatatua shida zinazoikumba hospitali hiyo.
Muungano huo unataka mfumo mzima wa hospitali kuchunguzwa, ikiwemo kuboresha mfumo wa kunakili data ya wagonjwa na pia kuongezwa kwa idadi ya maeneo ya upasuaji.



Wagonjwa wanavyoteseka kutokana na mgomo wa madaktari Kenya

Oroko alitetea uamuzi wa madaktari kususia kazi, akisema 'huu ndio wakati bora wa kuangalia kwa undani hali ya hospitali ya Kenyatta'.
Wiki iliyopita, Afisa mkuu mtendaji wa hospitali ya taifa ya Kenyatta mjini Nairobi - Lily Koros - alipewa likizo ya lazima huku Daktari na wahudumu katika hospitali hiyo wakisimamishwa kazi baada ya mgonjwa kufanyiwa upasuaji wa kichwa kimakosa.
Mkasa huo ulitokana na mchanganyiko wa majina ya wagonjwa wawili wote waliokuwa wana matatizo ya kichwa, na kosa halikujulikana hadi mgonjwa mmoja alipopasuliwa kichwa ndani ya chumba cha upasuaji.

Hospitali kuu ya KenyattaHaki miliki ya pichaAFP/GETTY

Muungano huo pia unadai marupurupu ya madaktari wakuu, ambayo wanasema hawajalipwa licha ya makubaliano na serikali mwaka jana.
Ni mwaka jana tu ambapo madaktari nchini Kenya waligoma kwa miezi mitatu wakidai kuboreshwa kwa hali za maeneo yao ya kazi sawa na mishahara.
Hospitali ya Kenyatta ndio hospitali kubwa zaidi ya umma nchini Kenya, na kusimamishwa kwa shughuli za matibabu huenda kukaathiri shughuli katika hopsitali nyingine nchini.
Takwimu zinaonyesha kuwa hospitali ya Kenyatta huwapokea wagonjwa wasiopungua 3,000 kwa siku.

Mada zinazohusiana