SERIKALI imesema, ni utashi wa kampuni za mafuta na nguvu ya soko kuwezesha uwekezaji wa biashara ya mafuta katika viwanja vya ndege.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kuandikwa amesema leo bungeni mjini Dodoma kuwa, sera ya uwekezaji katika viwanja vya ndege inatoa fursa ya kuuza mafuta ya ndege kwa kampuni binafsi yenye leseni ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA).

Amezitaja kampuni binafsi zenye leseni hizo na zilizoingia mikataba ya biashara na TCAA ni PUMA, OILCOM, TOTAL na PRIME FUELS.
Ameyasema hayo wakati anajibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Ritta Kabati aliyetaka kufahamu ni lini uwanja wa ndege wa Nduli utajengwa kwa kuwa upo kwenye mpango wa serikali wa ujenzi wa viwanja 11 vya ndege.
Mbunge huyo pia alitaka kufahamu ni utaratibu upi unaoutumika ili kuwe na kituo cha mafuta katika uwanja huo.
“Kwa sasa kiwanja hiki hakina ndege za kutosha zinazoweza kuvutia uwekezaji wa kituo cha mafuta” amesema Kuandikwa kwenye kikao cha kwanza cha Mkutano wa 11 wa Bunge la Tanzania.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, kiwanja cha ndege cha Nduli mkoani Iringa ni miongoni mwa viwanja 11 vya ndege vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina uliomalizika Mei mwaka jana.
Alisema, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali ilitenga fedha za ndani kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa kiwanja hicho ikiwa ni pamoja na kutangaza zabuni.
“Aidha kutokana na Benki ya Dunia kuonyesha nia ya kufadhili ujenzi wa uwanja huu, Serikali ilisitisha taratibu za ndani za manunuzi ili kusubiri manunuzi kufanyika kwa kuzingatia taratibu za Benki ya Dunia”amesema.