MJI wa Serikali ambao utakuwa na ofisi, makazi ya viongozi, mabalozi na taasisi za serikali makao makuu ya nchi Dodoma unatarajia kugharimu Sh trilioni 10.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uuzwaji wa viwanja zaidi ya 10,864 katika maeneo ya Mtumba na Iyumbu. Alisema mji huo unatarajia kujengwa na kukamilika ndani ya miaka 10 na utagharimu Sh trilioni 10.
“Utakuwa ni mji ambao utajumuisha ofisi za taasisi za serikali, wizara na mabalozi na makazi ya viongozi utakaokuwa na huduma zote za kijamii na uwekezaji wa majengo ya kisasa ya biashara na huduma ya usafiri wa treini ndani ya mji huo,” alisema.
Mji huo utakaojengwa eneo la Mtumba katika Kata ya Mtumba, Tarafa ya Kikombo, lina ekari 1,524 sawa na hekta 617 na lipo umbali wa kilometa 30 nje kidogo ya mji wa Dodoma. Alisema wako katika hatua za mwisho za kukamilisha plani ya mpango mji mpya na kwamba muda wowote wanaingia mikataba na wakandarasi.
Mpaka kukamilika kwake kinatarajia kuchukua miaka 10 na kugharibu Sh trilioni 10. Aidha, Kunambi alisema mpaka sasa tayari wamepokea maombi kutoka baadhi ya nchi wakiomba maeneo kwa ajili ya kujenga balozi zao na kutaja baadhi kuwa ni Uganda, Malawi, Zambia, China na Marekani.