RAIS wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amesema amani ni uhai wa nchi na wananchi kwani pasipo na amani ni vigumu hata kufikiri mambo yatakavyokuwa.
Mwinyi ameyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa viongozi mbalimbali wa dini, uliondaliwa na Kamati ya Amani mkoani humo.
Mwinyi amesema Tanzania kama sehemu ya jamii ya kimataifa inaishi katika uhalisia wakuwepo katika dini mbalimbali, na kwa miaka mingi imejulikana kama kisiwa cha amani.
“Viongozi wa dini wamefundisha amani, wameilea amani katika mzunguko mzima wa maisha. Pia wameunda majukwaa kwa ajili ya kuienzi amani".
Amesisitiza kuwa, Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam, imekuwa ikihamasisha viongozi wa dini na vyama vya siasa kutetea amani, hivyo ina kazi kubwa katika kuitetea amani.
Amesema, kwa msingi wa kamati hiyo, anaunga mkono iweze kusogea mbele ili ifike kwa kila mtu bila kujali dini wala hadhi yake.
Ameunga mkono dhamira ya kuikuza kamati hiyo badala ya kuwa ya Mkoa wa Dar es Salaam pekee, iwe ya taifa na iweze kusogea katika mikoa mingine, wilaya na hata vijiji.
Awali, Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Kanisa la Anglican, Jackson Sosthenes alisema amani ikitoweka nchini watakaoathirika ni watoto na wanawake, na kwamba ipo gharama ya kuirudisha.
“Viongozi wa dini na serikali tuangalie viashiria vya ukosefu wa amani ili tuweze kuimarisha. Katika tofauti zetu tunapaswa kuvumiliana kwa sababu thamani ya amani ni kubwa kuliko tofauti tulizonazo,” amesema.
Shehe Ally Muhidin aliishauri serikali kuangalia chembe ndogo ndogo za kudhibiti vinginevyo moto ukiwa mkubwa itashindikana kuudhibiti.
Kwa upande wake, Shehe Mkuu wa Tanzania, Shehe Abubakary Zubery alisema hakuna maisha bila amani, na kwamba neno amani linapaswa kurudiwarudiwa kwenye nyumba ya ibada, majukwaani na majumbani kwetu.
Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema tangu mwaka 2011, waliweza kuweka mahusiano baina yao viongozi mbalimba wa dini kwenye madhehebu mbalimbali na wapo mahali pazuri.
|
0 Comments