Goli la Penati lilofungwa na Cristiano Ronaldo katika dakika za majeruhi limeiingiza Real Madrid katika nusu fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Penati hiyo ilikuja baada ya Medhi Benatia katika mazingira yenye utata kumdondosha Lukas Vazquez kwenye eneo la hatari.
Ni katika mazingira hayo hayo, kwa kile kilichosemwa kuwa ni matumizi ya lugha mbaya, mlinda mlango wa Juve, Gianluigi Buffon katika ile ambayo inaweza kuwa Champions League yake ya mwisho alitupwa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi muingereza Michael Oliver.
Real, washindi mara tatu wa Ligi ya mabingwa Ulaya katika misimu minne, waliingia katika mechi hiyo ya mzunguko wa pili wakiongoza kwa mabao 3-0 lakini viongozi hao wa Seria A walianza kupoteza matumaini pale Mario Mandzukic aliposukuma kichwa nyavuni kutoka kwenye mkwaju ulionyunyizwa na Sami Khedira dakika mbili tu tangu kuanza kwa mchezo. Huyo huyo Mandzukic akapata goli la pili kupitia kichwa muda mfupi kabla ya kukamilika kwa kipindi cha kwanza.
Blaise Matuidi akafunga la tatu kutokana na makosa yaliyofanywa na Keylor Navas na hivyo kuifanya Juventus iwe na matokeo sawa na Real Madrid, jambo ambalo lingeipeleka mechi katika dakika za nyongeza kama siyo tukio la Penati lililotokea na kuifanya Real Madrid kutinga nusu fainali katika mazingira ambayo mashabiki wao walikuwa tayari wamekata tamaa.
Sasa, Real inaungana na Liverpool, Roma na Bayern katika droo ya timu nne zilizosalia, droo itakayofanyika Nyon, Uswisi, Ijumaa.
Bayern wao wametinga nusu fainali kwa maara ya saba katika miaka tisa baada ya kumaliza mechi yao dhidi ya Sevilla kwa matokeo ya bila kufungana lakini wakiwa na magoli mawili kibindoni dhi ya moja la Sevilla katika mechi ya mzunguko wa kwanza.
|
0 Comments