MBUNGE wa Jimbo la Ukonga (CHADEMA), Mwita Waitara amemuomba Rais John Magufuli kulimulika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), akidai kwamba linajiendesha kwa hasara na kushindwa kuwahudumia wananchi ipasavyo.


Waitara amesema hayo Bungeni jijini Dodoma leo na kulitaka shirika hilo kuharakisha utekelezaji wa miundombinu ya umeme ili kuwafikishia nishati hiyo wananchi walioko mjini na vijijini.

Mbunge huyo amedai kuwa hata jimboni kwake, Ukonga ambalo lipo ndani ya jiji la Dar es Salaam kuna maeneo mengi ambayo Tanesco bado hawajafikisha umeme huku akiomba gharama za kuweka umeme zipunguzwe kwa watu maskini walioko mjini kama ilivyo kwa wale wa vijijini.

“Wananchi wanapesa zao, wanalipia umeme lakini wanamaliza hadi miezi sita hawajafungiwa umeme, wakiuliza wanaambiwa hakuna nguzo, TANESCO ni Shirika la kibiashara, wameshindwa kufanya biashara, inabidi kuwepo na makampuni au mashirika mengine ya kuzalisha umeme ili kuwepo na upinzani kibisahara na Tanesco.

“Haiwezekani shirika ni la kwetu wenyewe, kodi wanalipa Watanzania halafu TANESCO ikajiendesha kwa hasara. Huwezi kwenda kwenye umeme wa viwanda iwapo hata umeme wa majumbani hauna. Lazima uwepo mpango mahsusi umeme umwekwe mjini na vijijni, anayetaka awekewe, asiyetaka abaki kwenye giza. Kuna mafisadi wengi, hawa watu washughulikiwe na haya maeneo ndiyo Rais Magufuli anatakiwa ayashugulikie,” alisema Mwita.