Bondia wa Kenya Fatuma Zarika anasema mpinzani wake kutoka Mexico, Yamileth Mercado, yuko mjini Nairobi kama mtalii.
Hivyo basi Fatuma anamshauri Mercado ajionee mbuga za wanyama wa pori na kufurahia mandhari safi ya jiji kuu la Kenya lakini asiwe na matumaini ya kuibuka mshindi Jumamosi ya Septemba tarehe 8 wakati Zarika atatetea ubingwa wake wa dunia wa chama cha WBC uzani wa super-bantam.

Fatuma Zarika akipimwa uzani
Pigano hilo litafanyika nje ya jumba la mkutano ya kimataifa la KICC kuanzia saa kumi na mbili za jioni za Afrika Mashariki.
``Namkaribisha Nairobi kwa moyo mkunjufu, afurahie nchi yetu, tunapenda wageni sana,'' anasema Zarika ambaye anatetea mkanda wake wa WBC kwa mara ya pili, mara ya kwanza ikiwa ni mwaka jana alipomshinda Catherine Phiri wa Zambia kwa pointi mjini Nairobi.
Fatuma zarika asema mpinzani wake atapa kipigo
``Mimi sijashindwa nyumbani kwa hivyo sitakubali nipoteze kwa mpinzani wangu wa Mexico kwa sababu nina uzoefu kumshinda na nimepigana na mabondia walio na ujuzi sana.''
Mercod Yemithi akipimwa uzani
Zarika kufikia sasa ameshinda mapigano 30, 17 kwa knockout akapoteza 12 na kwenda sare mara mbili, huku Mercado ameshinda mapigano 12, manne kwa knockout na akapoteza mara moja.
Namuuliza Zarika kama ananuia kumshinda Mercado kwa KO:``Hiyo ni siri yangu siwezi kusema hayo lakini atapata kipigo. Sitakubali kushindwa mbele ya mashabiki wangu wa nyumbani,'' anasema Zarika ambaye ana umri wa miaka 33 naye Mercado ana miaka 20.
``Najua kuna wengine wanasema kwa vile mpinzani wangu ana umri wa chini ana nafasi nzuri ya kunishinda lakini umri si neno hapo, la mhimu ni ujuzi ambao niko nao kumshinda.''
mabondia wote wawiuli wameahidi mchezo wa kutumbuiza
Mercado anasema ana mheshimu sana Zarika lakini anamuonya Jumamosi atakiona cha mtema kuni kwani atampondaponda vilivyo bondia wa Kenya, akitoa wito kwa madaktari wajiandae kumkimbiza Zarika hospitalini kwa sababu atamkomesha.
``Nimejiandaa vya kutosha, niko tayari kabisa kupambana na Zarika,nitamfunza adabu mbele ya mashabiki wake wa nyumbani,'' anasema Mercado kwa lugha ya Kihispania huku mkufunzi ambaye pia ni mkalimani wake Alfredo Leon akitufafanulia zaidi.