RAIS John Magufuli amepingana na sera ya serikali ya uzazi wa mpango akidai kuwa sera hiyo inapunguza nguvu-kazi kwa taifa na kuwataka wananchi wafanye kazi ili kukidhi mahitaji ya familia zao bila kujali idadi.

Ameyasema hayo jana, Septemba 9, 2018 akiwa mjini Meatu katika mkoani wa Simiyu huku akiongeza kuwa Watanzania waendelee kuzaa lakini wachape kazi ili kukidhi mahitaji ya watoto wao.

”Najua Waziri wa Afya Ummy Mwalimu hapa angependa kuongelea mambo ya uzazi wa mpango lakini mimi mengine huwa sikubaliani nayo sana, utapangiwaje kuzaa?  Najua kesho watapinga sana lakini ukweli ndiyo huo watu wamejazwa mawazo ya ajabu, huwezi kuwa mwanaume kisha ukubali kufungiwa kizazi! Yaani ng’ombe wako umtoe kizazi na wewe tena ukatolewe kizazi? Mimi sikubali’,’ alisema Magufuli.
Aidha, Magufuli amesema baadhi ya nchi barani Ulaya zinaujutia mpango huo kwani umezikosesha nguvu-kazi ya taifa huku akitolea mfano katika nchi mbalimbali alizowahi kuzitembelea ambazo zimekumbwa na tatizo hilo.