Familia ya bilionea aliyetekekwa nchini Tanzania Mohammed Dewji imevunja ukimya na kusema watatoa kitita cha Sh1 bilioni kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazopelekea kupatikana kwa bilionea huyo.

Katika mkutano na waandishi wa habari hii leo, mwanafamilia na mfanyabiashara maarufu Azim Dewji amesema familia itazichukulia taarifa hizo kuwa kama za siri na pesa hiyo itakuwa zawadi kwa atakayezitoa.
"…Familia inashukuru sana watu wote kwa kuendelea kututia nguvu na kumuombea kijana wetu Mohammed apatikane. Tunafarijika na ushirikiano na mshikamano wenu," amesema Azim Dewji na kuongeza, "Familia inapenda kutangaza zawadi ya Sh1bn kwa atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake."
Familia hiyo pia imetoa shukrani kwa serikali na vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwa hatua wanazochukua katika kumtafuta Mohammed (Mo) Dewji.
Bwana Azim hatahivyo hakuwa tayari kupokea maswali ya waandishi akisema nguvu ilekewzwe katika kumuombea Mo apatikane.
Mo DewjiHaki miliki ya pichaAFP/GETTY
Mo, 43, ni Mtendaji Mkuu wa kundi la Makampuni ya Mohammed Enterprises Limited (MeTL) alitekwa nyara na watu wasiojulikana Alhamisi ya wiki iliyopita akiwa anaelekea mazoezini jijini Dar es Salaam.
Mpaka sasa bado haijajulikana ni nani hasa aliyemteka japo mamlaka nchini Tanzania zinsema kuwa tukio hilo liliongozwa na raia wawili wa kigeni.
Tayari watu 30 wanashikiliwa kutokana na tukio hilo japo bado haijafahamika ni ipi hasa sababu ya kutekwa kwa tajiri huyo na wapi alipofichwa.
Mo anakadiriwa na jarida la masuala ya fedha la Forbes kuwa na utajiri wa dola bilioni 1.5 na kuwa mtu tajiri zaidi Afrika Mashariki na bilionea mdogo Zaidi kiumri kwa Afrika.