BAADHI ya wananchi wa kata ya Pangani ,Kibaha Mjini mkoani Pwani, wakiwa kwenye mkutano wao kuhusu serikali ya wilaya na mkoa kuangalia namna ya kufuta umiliki wa mashamba makubwa ambayo hayaendelezwi na kusababisha kutumika kama vificho vya wahalifu na kuokotwa miili ya wafu na walionusurika kufa.NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA 


BAADHI ya wananchi wa kata ya Pangani ,Kibaha Mjini mkoani Pwani, wameitaka serikali ya wilaya na mkoa kuangalia namna ya kufuta umiliki wa mashamba makubwa ambayo hayaendelezwi na kusababisha kutumika kama vificho vya wahalifu na kuokotwa miili ya wafu na walionusurika kufa.

Wameeleza kwa kipindi cha miezi sita miili zaidi ya kumi zimeokotwa kwenye mtaa huo ambapo kati yao wengine walinusurika kifo na kuokolewa na wengine wakiwa wamefariki dunia. 


Diwani wa kata ya Pangani , Agustino Mdachi aliyasema hayo kufuatia mwili wa mtu mmoja mwanaume aliyekufa kuokotwa kwenye mtaa wa Pangani .Alieleza ifikie wakati wamiliki hao wasiangaliwe nyadhifa ama majina yao ili kunusuru maisha ya watu. "Miili ya watu imekuwa ikiokotwa mara kwa mara,wengine wanaookolewa wakiwa wametupwa hivyo tunaitaka serikali kuyafutia hati mashamba haya ili yagawiwe kwa wananchi waweze kuyaendeleza likiwemo shamba la serikali la mifugo la Mitamba", alisema Mdachi.

Hata hivyo Mdachi alisema ,wameshachukua hatua ya kuwaita wamiliki wa mashamba hayo ili kuwaeleza vitendo vinavyotokea lakini baadhi yao wamekuwa hawajitokezi .

Nae mwenyekiti wa mtaa wa Pangani Jitihada Ndiali alisema,eneo hilo kwa sasa limefanywa kama dampo au sehemu ya kutupia maiti pia madereva bodaboda kuporwa pikipiki zao kisha kutupwa .Mwenyekiti wa mtaa wa Miwale ,Amos Mkwawa alisema kuwa maeneo hayo pia ni changamoto kwa wanafunzi wa kike ambao wapo hatarini kubakwa.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka aliwaomba wamiliki husika kujitokeza kwenda kuyaendeleza maeneo yao. Jitihada za kumtafuta kamanda wa polisi mkoani Pwani (ACP )Wankyo Nyigesa ili aeleze ama kuthibitisha kuhusu maiti hiyo iliyookotwa hazikuzaa matunda kutokana na kuwa kikaoni.