Waziri mpya wa Kilimo nchini Tanzania Japhet Hasunga ameiambia BBC kuwa serikali itafikiria hatima ya wafanyabiashara wa korosho mara baada ya kumaliza ununuzi wa zao hilo.

Hasunga amewasili leo mkoani Mtwara mara baada ya kuapishwa na rais John Magufuli jana Ikulu jijini Dar es Salaam kuchukua nafasi ya Charles Tizeba aliyefutwa kazi kutokana na kadhia ya korosho.
Rais Magufuli jana alitangaza rasmi kuwa serikali itazinunua korosho zote kwa kupitia benki ya kilimo na uratibu wa jeshi baada ya wafanyabiashara kuonekana wakisuasua.
"Hatima ya wafanyabiashara wa korosho labda wasuburi tukishanunua hizi korosho ndio tutakaa nao tuamue. Tulishakaa nao vikao vingi, tukakubaliana na bei elekezi, wao hawakutaka kuzingatia. Wanadhani serikali labda hatuwezi ndio maana tunanua wenyewe sasa, halafu ndio tufikirie sasa namna ya kushirikiana nao," amesema Hasunga na kuongeza: "Tunajua kuwa wanaumuhimu, lakini si umuhimu wa kuringa ama kutaka kununua kwa shilingi 1,500 au 2,000..."
Hasunga pia amesema maamuzi ya serikali yanalenga kuongeza kipato kwa mkulima, kutoa ajira mpya kwa kuzibangua korosho ndani ya nchi na pia kuliongezea thamani zao hilo kwa kulifungasha kabisa kabla ya kusafirisha nje ya nchi na kuongeza pato la taifa.
Waziri huyo amesema kuwa wanajeshi wanatarajiwa kuwasili muda wowote hii leo kuanza kuratibu mfumo mpya wa manunuzi ya zao hilo.
Hali imepoa kidogo leo Mtwara hakuna kazi
Image captionHali imepoa kidogo leo Mtwara hakuna kazi
Awali, wanawake wajasiriamali wanaoshughulika na kubangua korosho nchini Tanzania wameulalamikia mpango mpya wa ununuzi uliotangazwa.
Wanawake hao wanasema kuwa hatua hiyo itawanyima fursa ya ununuzi wa kiwango cha kawaida kwa lengo la biashara ndogo ndogo kwani, wana wasiwasi kwamba huenda jeshi likabadili kabisa mfumo wa uuzaji korosho tofauti na walivyozoea.Hapo jana ikiwa ni kabla ya muda uliowekwa kwa wafanyabiashara kujiorodhesha ili wanunue korosho ya wakulima mkoani Mtwara, rais alibadili mawazo yake na kuamua kwamba wafanya biashara hao hawatanunua tena korosho hiyo, akihoji kwamba walikuwa wapi.
"Yani huu mpango ambao rais ameuweka katika uuzaji wa korosho Mtwara kusimamiwa na jeshi, sisi wafanyabiashara wadogo kiukweli wametuangusha", amedai mmoja wa wanawake ambaye ni maarufu kwa biashara hiyo.
"Mimi ni mjasiriamali mdogo ambaye nnanunua gunia moja au mbili katika kipindi cha msimu wa korosho , nabangua na kuuza. Sasa wameweka usimamizi wa jeshi , nitanunua wapi? Nina miaka 15 ninafanya hii shughuli nnaendesha maisha na nnasomesha watoto"... amelalamika mjasiriamali mwingine mwanamke.
koroshoHaki miliki ya pichaISSOUF SANOGO
Leo ni siku ya pili Baada ya serikali ya Tanzania kukabidhi Jeshi la nchi hiyo, kuratibu shughuli za ununuzi wa korosho katika mkoa ulioko Kusini mwa nchi hiyo, Mtwara. Hatua hiyo inafuatia Rais John Magufuli kusitisha mpango wa makampuni kununua zao hilo kwa kile alichodai wamekuwa na bei hazina tija kwa wakulima .
"Kiukweli nimevurugwa kwa msimamo huu uliowekwa, kwa sababu sisi ni wajasiriamali wadogo ambao hatuna uwezo wa kununua tani moja, tani mbili ..tunajikwamua tu kidogo kidogo.
Wanasaidiwa wakulima lakini sisi wajasiriamali wadogo wadogo tutaishije?"
Kwa sasa korosho zinauzwa kwa gharama ya shilingi 3,300 badala ya shilingi 3000 za kitanzania ambayo ni sawa na dola 1.43.
Jumamosi, Rais Magufuli aliwatimua mawaziri wawili katika baraza lake, Waziri wa Kilimo Charles Tizeba na Waziri wa Biashara Charles Mwijage.
Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe MagufuliHaki miliki ya pichaAFP
Image captionRais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
Rais amesema anataka kuhakikisha maelfu ya wakulima wanapata faida kwa mazao yao na kuhakikisha kipato kutokana na usafirishaji wa korosho katika mataifa ya nje.
Lakini wakosoaji wanasema huenda ni hatua ya kujaribu kutafuta uungwaji mkono katika eneo la Mtwara, eneo lililo ngome ya upinzani.
Mwansiasa wa upinzani Zitto Kabwe amesema serikali inastahili kupata ridhaa ya bunge kununua korosho hizo.
Kadhalika rais Magufuli ameivunjilia mbali bodi ya usimamizi wa zao la korosho Tanzania na kutegua uteuzi wa mwenyekiti wake, Anna Abdallah.