Wahenga walilonga kuwa “Kimya kingi kina mshindo mkuu” msemo huu ameudhihirisha nguli wa miondoko ya rhumba Bozi Boziana.
Nguli huyu amerudi tena kwenye dimba la muziki, hivi sasa hupo bize studio akitayarisha ngoma mpya yenye jina la ‘Android’.
Kwenye ngoma hiyo amemshirikisha Ferre Gola ‘Le Padre’, mwanamuziki ambaye hivi sasa ni gumzo katika jiji la Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa uhodari wa kuimba na kunengua.
Kabla ya ngoma hiyo, nguli huyo awali alifanya onesho kabambe akishirikiana na wakali wenzake, akina General Defao, Scola Miel, MJ 30 na Celenzino.Bozi alikuwa kimya pasipo kupakua wimbo wowote kwa kipindi kirefu, akijiandaa kufanya makubwa.
Licha ya umri wake wa miaka wa miaka 67, bado anao uwezo mkubwa wa kutunga na kuimba nyimbo za muziki wa dansi.Bozi Boziana alijipatia umaarufu wakati akisikika akirap maneno ya “Nzawisaa, Nzawisaaa maama Nzawisaaa..Yelooh!!!” kwenye nyimbo za bendi yake.
Ukimuita kwa jina la Mbenzu Ngamboni Boskill, hautakuwa umekosea kabisa kwa kuwa ndiyo aliyopewa na wazazi wake baada ya kuzaliwa.
Bozi Boziana alizaliwa mwaka 1952 huko Jamhuri ya Kidemkokrasia ya Kongo.
Katika hatua za kutafuta mafanikio, Boziana alipitia katika bendi nyingi kubwa na ndogo nchini mwake zikiwa ni pamoja na Bamboula de Papa Noel, Minzoto Sangela, Zaiko Langa Langa, Isifi Lokole, Yoka Lokole, Langa Langa Stars na Choc Stars.
Baadhi ya wapenzi wakampachika jina bandia la ‘Mzee Benzi’ ambalo limekuwa maarufu.Katika kutafuta njia ya kujikwamua kimaisha, Bozi Boziana aliamua kuunda bendi yake ya Orchestra Anti-Choc, ambayo anaiongoza hadi sasa.
Licha ya utunzi na uimbaji, pia ni mkung’utaji mzuri wa gitaa na kulishambulia jukwaa akishirikiana na akina dada wawili Betty na Scolla Miell.
Mzee Benzi alianzia muziki wa Afro-Pop katika bendi ya Air Marine. Lakini alianza kuyaona mafanikio ya kazi zake ilipotimu mwaka 1974 alipojiunga na bendi ya Zaiko Langa Langa, hivi sasa bendi hiyo inaongozwa na Nyoka Longo.
Zaiko LangaLanga ilikuwa na waimbaji mashuhuri wakati huo wakiongozwa na mkongwe Papa Wemba na mwezake Evoloko Jocker.
Lakini haikuzidi mwaka, Papa Wemba na Evoloko waliondoka bendi hiyo baadae hata Bozi Boziana aliwafuata kwenda kuanzisha bendi mpya ikaitwa Isifi Lokole.
“ Fahari wawili hawakai zizi moja” usemi huo ulijidhirisha baada ya wanamuziki hao kushindwa kukubaliana katika maswala mbalimbali ya msingi yaliyopelekea wanamuziki wake akina Papa Wemba, Boziana, Mavuela Somo na wengine kuondoka bendi ya Isifi Lokole.
Walienda kuunda bendi yao mpya iliyopewa jina la Yoka Lokole.
Bendi ya Yoka Lokole ilipata mafanikio makubwa mwaka 1976, japokuwa ilipotimu mwinshoni mwa mwaka huo, Papa Wemba aliiacha bendi hiyo, akaenda kuanzisha bendi ya Viva la Musica.
Bozi Boziana mwaka 1977 naye aliicha bendi hiyo ya Yoka Lokole, licha ya bendi hiyo kuwa maarufu kwa kipindi kifupi.
Kwa miezi michache Boziana alishirikiana na mwanamuziki Efonge Gina, ambaye naye alikuwa katika bendi ya Zaiko Langa Langa.
Walirekodi nyimbo kadhaa kama vile Selemani iliyotungwa na Bozi Boziana na Libanko Ya Ngai utunzi wake Gina.
Mwanamuziki aliyekuwa na uwezo mkubwa wa fedha Kiamuangana Mateta ‘Verkies’ mwaka 1981, aliibadilisha bendi ya Soukous Super Group na kuiita Langa Langa Stars.
Bendi hiyo ilikuwa imesheheni vipaji vya wanamuziki kaiwemo Evoloko Jocker, Dindo Yogo na wengine wengi.
Bozi Biziana alialikwa kujiunga na vijana hao, pasipo kusita akaukubali na kuicha Zaiko Langa kwa mara ya pili.
Langa Langa Stars ilidumu kwa miaka michache iliyofuatia kabla na Boziana naye akaondoka kwenda kujiunga na bendi kubwa nchini humo ya Choc Stars, aliyokuwa chini Ben Nyamabo ambako alipiga hadi mwezi Novemba 1985.
Akiwa na bendi hiyo ya Choc Stars, Boziana alirekodi baadhi ya nyimbo ambazo zilikuja kuwa maarufu za Sandu Kotti, Alena, Mbuta-Mutu na Retrouvailles a Paris.
Choc ilikuwa na wanamuziki wengi wenye vipaji lukuki wakiwemo akina Fifi Mofude, Djo Nolo, Koffi Alibaba, Wally Ngonda, Rigo Star, Ngouma Lokito, Deesse Mukangi, Marthe Lamugenia, Ngimbi Yespe na Maoussi Solange.
Mpiga gita wa kwanza katika bendi hiyo alikuwa Matou Samuel ambaye kwa sasa anaimba muziki wa Injili na nafasi yake ilishikwa na Dodoly ambaye kabla ya kujiunga humo alitokea katika bendi ya mwanamuziki Lita Bembo ya Orchestre Stukas.
Dodoly alipachikwa jina bandia la ‘The sewing machine’ kwa umahiri wake wa kutumia vidole vyake kucharaza nyuzi kwa kasi kubwa.Tokea miaka ya 1980 Boziana aliendelea katika bendi yake ya Anti-Choc ikiwa ni pamoja na kurekodi nyimbo akishirikiana na wanamuziki wengine mahiri.
Boziana aliwahi kushinda zawadi ya Kora All-African kwa album yake kuwa bora toka nchi za Afrika ya Kati.
Wapenzi wa muziki hapa nchini watamkumbuka Bozi jinsi alivyoziteka nyioyo za wapenzi katika maonesho kadhaa aliyoyafanya hapa nchini.
Alifanya maonesho kadhaa akishirikiana na wasanii wake wa kike Deesse Mukangi na Joly Detta walivyokuwa wakiimba na kulishambulia jukwaa kwa mtindo wao wa ‘Nzawisa’ katika nyimbo za Tembe na Tembe, Palpitation na zingine nyingi zilifanya watu kuviacha viti vyao kwenda kuwatuza.
Bozi Boziana mwenye sauti nzuri yakupendeza, kuna kipindi alibadili dini yake na kuwa muislamu, akapewa jina la Abubakar.
Baadhi ya nyimbo alizowahi kufyatua ni pamoja na Masumu Akey, Mitshuri, Mbuza, Ba Bokilo, Benson Nostalgique, Mon Mari Est Gabonais na Pere Noelle Confiance.
Zingine ni Fiko Fikolo, Chama Chiko, Mya , Ka Munu Ve’, Mifune, Popy Bopase ya mwaka 1998 na Tembe na Tembe.Zingine ni Bana DRC, Riana, Anytha, Sonto ya 1989, Makambo Evelyn ya mwaka 1989, Pot Pourri , Mfumu na Alena.
Bozi alachia vibao vingine vya Sisina, Doukoure, Switzerland, Wakamba, Mansanga na Betlem.Mzee Benzi alifyatua vibao vingi mno vilivyompa sifa nyingi ukiwemo wa La reine de Sabah, Lelo Makambo Lobi na Fleur de Lys ambazo alimshirikisha mwimbaji wa kike Joly Delta.
Watanzania watamkumbuka alivyofanya mambo makubwa katika muziki kwa mara ya mwisho alipokuja humu nchini kwa mwaliko wa Kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET) iliyo chini ya uongozi wa Mkurugenzi Asha Baraka.
Bozi Boziana ni mfano wa kuigwa jinsi anavyoweza kutulia, baadaye anatoka na nyimbo zainazokubalika na kudumu masikioni mwa wapenzi wa muziki huo.
Hii ni tofauti sana na wanamuziki na wasanii wetu, ambao ‘huopoa chakula watu wale hata kabla hakijaiva!.
Na Moshy Kiyungi,Dar es Salaam.
|
0 Comments