RAIS  John Magufuli amewaapisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Lugha Bashungwa, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Edwin Mhede na Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Charles Kichere.

Pia, Magufuli amepokea gawio la Tsh bilioni 3 kutoka kampuni ya mawasiliano ya Bhart Airtel ambayo inamilikiwa  na serikali kama mwanahisa na Tsh bilioni 2.57, ambayo wamekabidhi ikulu kama pongezi kutokana na mambo makubwa yanayofanywa na serikali.


“Ni historia kwa mazungumzo yaliyofanyika kati ya serikali na Bhart Airtel. Wapo waliodhihaki, wapo waliocheka, wapo waliojua hiki hakiwezekani, lakini nafikiri wote waliotutakia mabaya Mungu amewaumbua. Tumeingia mazungumzo usiku na mchana na yakafikia mahali mkakubaliana, nawapongeza nyinyi na Airtel.

“Miaka 19 yote iliyopita imepita free, hatukupata ‘divident’ yoyote, sitaki kulaumu miaka ile iliyopita hapakuwa na wataalamu kama hawa walioshiriki kwenye mazungumzo, nasema ni historia. Tulikuwa na asilimia 40 lakini bado hatukupata chochote.

“Hizi fedha zitakazoingia wala haziingii kwenye mfuko wa Magufuli, zinaenda kwa Mheshimiwa Philipo,  ndugu yake na John zikatumike kwa Watanzania, kwani ningewaambia kimyakimya hizo Tsh bilioni 2 na ushee wekeni kwenye akaunti yangu fulani, lakini nikasema waje wazitoe hapa hadharani. Hiyo cheki ya dola milioni 1 (bil 2.25) muikabidhi kwa Katibu Mkuu akaanze kujenga hospitali pale Dodoma.

“Fedha hizi tutakazokuwa tukizipata kama gawio kwa miaka mitano ni ukombozi wa hali ya juu kwa nchi yetu kwani itasaidia katika maendeleo mbalimbali nchini. Licha ya kutopata chochote kwa miaka 19 iliyopita, lakini tukabandikwa  deni la bilioni 930.

“Bilioni moja itakayotolewa kwa miaka mitano ni Tsh bil. 60, kituo cha afya kimoja kinagharimu Tsh. 400m, kwa Tsh bil. 60 ni zaidi ya vituo 100 vitajengwa na kuwahudumia wazee, watoto, wajawazito na wagonjwa wengine, nadhani ni kitu kikubwa sana.

“Natoa agizo kwa wanaohusika na ujenzi wa hospitali kuchukua fedha hizo zilizotolewa na Mwenyekiti wa Bharti Airtel kama mchango binafsi ili kuanza ujenzi wa Hospitali mpya jijini Dodoma,” alisema Magufuli.

TAZAMA TUKIO HILO HAPA