*Ni wale waliotajwa wakati wa kikao cha Rais Magufuli na wafanyabiashara

Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii

OFISA Msaidizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato nchini(TRA) Charity Ngalaw(28) na askari Polisi wawili wamepandishwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na shtaka la kuomba rushwa ya Sh. Milioni mbili.

Mbali Ngalawa, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Askari Polisi wa kituo cha Polisi Osterbay, H 4810 PC Ramadhani Uweza (28) na H 48 86 PC Simon Sugu (26).

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali kutoka Takukuru , Sofia Ngula amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa, Oktoba 29,mwaka 2016 huko Kimara Mwisho ndani ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam washtakiwa hao walishawishi rushwa ya Sh. Milioni mbili kutoka kwa mfanyabiashara wa Karikaoo jijini hapa, Ramadhani Ntunzwe , ili iwe kishawishi cha kuachia mizigo ya Mfanyabiashara huyo.

Kwa madai kuwa waliukamatwa kwa madai ya kufanya udanganyifu wa bidhaa alizonazo na hivyo kuathiri ukadiriaji wa kodi, kazi ambayo ni ya mwajiriwa wake.

Hata hivyo, washtakiwa wamekana shtaka hilo na wameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa na mahakama ambapo wametakiwa kuwa na mdhamini moja mwenye kitambulisho, atakayesaini bondi ya sh. Milioni tano.

Kwa mijibu wa upanda wa Mashtaka, upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na wako katika hatua za mwisho kukamilisha. Kesi imeahirishwa hadi Julai 10, mwaka huu.