Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.

WATU wanne wakazi wa sehemu tofauti jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shitaka la kuchapisha maudhui ya Youtube bila ya kuwa ba kibali kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Washitakiwa hao ambao wamefikishwa mbele ya mahakimu wanne tofauti mahakamani hapo ni Charles Kombe (24) mkazi wa Mikocheni, John Chuwa (28), mkazi wa Barakuda ,Amos Warema (27) na Raymond Mkoroka (30).

Wote kwa pamoja wanadaiwa kuchapisha mtandaoni maudhui hayo katikà tarehe tofauti kati ya mwaka 2018 na Mei mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Wakili wa serikali Elizabert Mkunde  amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Mbando  kuwa, kati ya Agosti 1 ,2017 na Mei 21, 2019 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam.
Mshtakiwa Kombe alichapisha maudhui hayo kupitia mtàndao wake wa Youtube  uitwao Charles Kombe bila kibali.

Hata hivyo, mshtakiwa Kombe amekana kutenda shitaka hilo na yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza sharti la kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh.milioni 5 kila mmoja.


Mshitakiwa chuwa, amesomewa shitaka lake mbele ya Hakimu Mkazi Maira Kasonde ambapo Imedaiwa, kati ya mwaka 2018 na Aprili 2019 jijini Dar es Salaam mshtakiwa alichapisha maudhui kupitia mtandao wa Youtube uitwao John film entertainment bila ya kuwa na kibali kutoka TCRA.


Mshtakiwa Chuwa amekiri kutenda kosa hilo na yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza sharti la kujidhamini mwenyewe kwa bondi ya sh milioni tano

Kesi imeahirishwa hadi Juni 7 mwaka huu mshitakiwa atakaposomwewa Maelezo ya awali.


Katika kesi nyingine mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Janet Mtega imedaiwa na wakili wa serikali Candid Nasua kuwa  kati ya Novemba 2018 hadi Mei 17 mwaka huu katika maeneo tofauti katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam mshitakiwa Warema

alisambaza maudhui hayo kupitia mtandao wa Youtube uitwao Pro Media Tanzania bila kuwa na kibali kutoka TCRA.


Mshitakiwa amekana kutenda kosa hilo na yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambapo mahakama ilimtaka  kujidhamini mwenyewe na kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya sh. milioni 3.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 4 mwaka huu na upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. 

Kwa upande wake mshtakiwa  Mkoloka alisomewa shitaka lake  na wakili wa serikali Elia Athanas mbele ya Hakimu Mkazi Rwezile.

Mshitakiwa amekana shtaka hilo na yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza sharti la kuwa na mdhamini mmoja na kujidhamini mwenyewe kwa kusaini bondi ya Sh. Milioni 5.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 4 mwaka huu itakapotajwa.