Mbunge wa Kondoa Vijijini (Naibu Waziri wa Fedha na Mipango), Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, akifafanua jambo kwa wananchi wa Kijiji cha Ihari ambapo aliahidi kuufikisha mgogoro wa ardhi wa Kijiji hicho kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Wiliam Lukuvi, kwa ajili ya utatuzi 
Mbunge wa Kondoa Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akimsikiliza kwa makini Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi – Ihari, Bw. Issa Juma baada ya mkutano wa hadhara. 
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kondoa, Dodoma, Alhaji Othman Gora akiwasalimia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ihari wilayani humo ambapo Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alikuwa mgeni rasmi.

Na Mwandishi wetu, Kondoa, Dodoma 


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameahidi kuupatia ufumbuzi mgogoro wa ardhi katika Kijiji cha Ihari wilayani Kondoa, baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi wanaoishi katika Kijiji hicho. 

Ahadi hiyo aliitoa wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji hicho ambapo wananchi na viongozi walipata nafasi ya kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili. 

Wananchi wa Kijiji hicho walieleza kuwa mgogoro huo umesababisha wengi wao kukosa mahala pa kuchungia mifugo yao kwa kuwa eneo lililokuwa limetengwa kwa ajili ya malisho limevamiwa na kubadilishwa matumizi kuwa mashamba. 

Dkt. Kijaji ambaye pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini, alisema taarifa za mgogoro huo ataziwasilisha kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi ili aweze kutatua changamoto hiyo ambayo imekuwa kero kwa wananchi hao. 

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni Serikali ya wanyonge na imepanga kutatua kero mbalimbali za wananchi ikiwemo migogoro yote ya ardhi nchini. 

Dkt. Kijaji aliwaomba wananchi hao wawe na Subira katika kipindi hiki ambacho Serikali inaenda kushughulikia tatizo lao huku akibainisha kuwa utatuzi wa mgogoro huo unategemea sana utulivu wao kama walengwa. 

“Niwaombe ndugu zangu tueendelee kuilinda amani ya Ihari, tuendelee kuilinda amani ya Kondoa na nchi yetu kwa ujumla katika kipindi hiki ambacho tunamsuburi Waziri wa Ardhi ambaye anajua matumizi ya kila kipande cha ardhi nchini, atatue mgogoro huu”, alisisitiza. 

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihari, Bw. Idi Lumba amemshukuru Dkt. Kijaji kwa kutenga muda wa kusikiliza changamoto zao hususan tatizo la ardhi ambalo lilianza kuwagawa wananchi wake. 

Bw. Lumba alimhakikishia Mbunge huyo kuwa hali ya Kijiji cha Ihari itaendelea kuwa tulivu kwa kipindi chote ambacho watakuwa wanasubiria suluhu ya mgogoro huo, huku akielezea changamoto ya maji na umeme katika Kijiji hicho ambazo Dkt. Kijaji aliahidi kuzitatua kwa haraka.