MWANAMUZIKI wa Bongo Fleva kutoka kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Mbwana Yusuph ‘Mbosso’ amemtoa machozi shabiki wake wa Mombasa nchini Kenya, Jamal Ismail a.k.a ‘Anacheza Anaona Raha’.

Mbosso amefanya jambo kubwa la kumsaidia Jamal ambaye alijikuta akitokwa na machozi kutokana na kukwama hospitalini baada ya kukosa fedha za kulipia matibabu.  Iko hivi; Jamal amekaa hospitalini yapata miezi miwili kabla ya kuruhusiwa wiki iliyopita baada ya kukatwa mguu wake mwingine na sasa hana miguu.


Jamal alikuwa amelazwa kwa muda huo wa miezi miwili katika Hospitali ya Coast General kutokana na matatizo ya kiafya yaliyohusisha mguu wake uliokuwa umebaki baada ya kupoteza wa awali na kuwa mlemavu wa mguu mmoja kwa muda mrefu huku familia yake ikishindwa kumnasua hospitalini.

Akilisimulia Ijumaa Wikienda kuhusu kisa chake na Jamal, Mbosso alisema kuwa aliamua kumlipia bili ya hospitalini baada ya kushindwa kufanya hivyo na kuendelea kukaa hospitalini.
Mbosso alisema auliunganishwa na Jamal na mwigizaji na mtangazaji wa Mombasa aliyemtaja kwa jina la Mama Madikodiko. “Mama Madikodiko amekuwa daraja muhimu kati yangu na Jamal,” alisema Mbosso na kuongeza; “Baada ya kumlipia Jamal deni lake la hospitalini alifurahi kiasi cha kutokwa na machozi.”

Hata hivyo, Mbosso aliahidi kuendelea kumsaidia Jamal kwa kumnunulia kiti cha matairi kwani sasa ana ulemavu wa kutokuwa na miguu. Alipoulizwa namna alivyokutana na Jamal, Mbosso alieleza; “Jamal alipata umaarufu iliposambaa video yake akiimba wimbo wangu wa Nipepee na hapo ndipo nilipoanza kumfuatilia.
“Nakumbuka wakati wa Tamasha la Wasafi mwaka jana kule Mombasa, nilimuita stejini na kweli alikiri kwamba ni shabiki wangu mkubwa.” Mbosso ameendelea kupongezwa kwa moyo wake huo na kwamba hiyo ndiyo maana halisi ya kurudisha kwa jamii.