Miongoni mwa masuala yaliyopata mjadala miongoni mwa jamii ya Tanzania baada ya ajali iliyotokea eneo la Msamvu mkoani Morogoro, ni pamoja na uchukuaji wa tahadhari pindi kunapotokea ajali ya aina hii.
Mwandishi wa BBC Aboubakar Famau amezungumza na Kamishna wa operesheni Jeshi la zimamoto na uokoaji, Bwana Billy J. Mwakatage katika kipindi cha Amka na BBC

Kumekuwa na tabia kwa watu kukimbilia maeneo yanapojulikana kuwa hatari imetokea, tabia ambayo imekemewa vikali na wataalamu wa Idara ya zimamoto.
Baadhi ya watu walikutwa na umauti walipokuwa wakichota mafuta yaliyomwagika baada ya lori la mafuta kupinduka mjini humo.
Lakini kwa nini tabia hii hujitokeza mara kwa mara?
Kamishna wa operesheni Jeshi la zimamoto na uokoaji, Bwana Billy J. Mwakatage akizungumza na Aboubakar Famau mjini Morogoro
Je, ni tahadhari za kuchua iwapo gari ya mafuta inakuwa kwa bahati mbaya imepatwa na ajali na kuanguka?
Kamishna Mwakatage anasema : ''Gari lolote likianguka ikiwa na shehena ya mafuta haipaswi kukaribiwa, mtu yeyote asiye mtaalamu hapaswi kusogelea, na si mafuta tu ni bidhaa nyingine zinazosafirishwa na vyombo vya usafirishaji kama sumu pamoja na kemikali hatari''.
Kamishna amesema sasa hivi sasa kuna mfumo wa utoaji elimu kuhusu namna ya kupambana na majanga ya moto, elimu inayotolewa kwenye shule mbalimbali
''Idara ya zimamoto imepita kwenye sule za msingi na sekondari tukiwafundisha. Tumeanzisha fire clubs zinazofundisha namna ya kuchukua tahadhari wakati wa majanga ya moto ili waelewe madhara ya moto pia tahadhari za kuchukua''.
''Na tumeanza kwa shule kwa watoto wadogo, kujua namba ya dharura, si tu kwa majanga ya moto, bali pia uokozi na mengine yote isipokuwa jinai kuwafundisha kuifahamu namba ya dharura ya jeshi la zimamoto na uokoaji, 114''. Alieleza kamishna.
Miili ikiwa kwenye majeneza tayari kuzikwa
Funzo kwa jamii
Matukio haya yamekuwa yakihatarisha na kupoteza maisha ya watu wengi. Kamishna Mwakatage anasema suala la kutoa elimu kwa Umma ni endelevu, si la mara moja kwani kujua kwa mmoja si kujua kwa mwingine.
Moja ya sababu ya madhara kuwa makubwa kiasi hiki ni tamaa ya kufikiri kuwa kuna chochote kinachoweza kumfaa mtu kutokana na ajali.
''Watanzania wanapaswa kujifunza kutokana na historia kwa kuwa tukio la moto si mara ya kwanza kutokea nchini Tanzania.Tukio kama hilo liliwahi kutokea mbeya eneo la Ntokela''.
''Tukio kama hili likitokea hasa magari yanayobeba mafuta na kemikali hatari hatutakiwi kuyasogelea isipokuwa wataalamu kwa ajili ya kuondoa hatari iliyo mbele''.
Pia alisema kuwa faraja kubwa inahitajika kwa walioathirika na tukio hilo kwa kuwapa msaada wa kisaikolojia kwa sababu janga lilikuwa kubwa na kuathiri akili kwa kuwa limeleta madhara na mbadiliko makubwa sana katika mfumo mzima wa maisha ya watu mjini Morogoro na kufanya mkoa mzima kuzizima.
Waombolezaji
Baadhi ya matukio ya mikasa ya malori ya mafuta Afrika
January 31 2009 Kenya: Moto uliwachoma watu waliokuwa wakifyonza mafuta wakati lori la mafuta lilipoanguka huko Molo kaskazini mwa mji wa Nairobi na kuwaoa watu 122.
Julai 2, 2010, DR Congo: Takriban watu 292 waliuawa wakati lori la mafuta lilipolipuka mashariki mwa kijiji cha Sange. Baadhi ya waathiriwa walikuwa wakijaribu kuiba mafuta baada ya ajali hiyo huku wengine wakitazama mechi ya kombe la dunia.
Oktoba 6, 2018 DR Congo: Takriban watu 53 waliuawa baada ya lori la mafuta kugongana na gari jingine na kushika moto katika barabara kuu ya mji mkuu wa Kinshasa
Septemba 16 2015 Sudan Kusini: Watu 203 walifariki na wengine 150 kujeruhiwa wakati watu walipokuwa wakijaribu kuiba mafuta.
Novemba 17 2016 Msumbiji: Takriban watu 93 waliuawa wakati lori la mafuta lililokuwa likibeba petroli lilipolipuka magharibi mwa taifa hilo . Mamia walikuwa wakijaribu kufyonza mafuta kutoka katika gari hilo.
Julai 12 2012, Nigeria: Takriban watu 104 walifariki walipokuwa wakijaribu kuchukua mafuta kutoka kwa lori la mafuta baada ya kuanguka kusini mwa jimbo la River State.
Oktoba 9 2009 , Nigeria: Takriban watu 70 walifariki kusini mashariki mwa jimbo la Anambra baada ya lori la mafuta kulipuka huku moto ikichoma magari kadhaa.