Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia- WB, Kanda ya Afrika, Bi. Anne Kabagambe, (wa pili kushoto), akiangalia ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa –SGR, kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro, kulia ni Mkurugenzi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Reli , Mhandisi Felix Nlalio.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia- WB, Kanda ya Afrika, Bi. Anne Kabagambe (kulia), akiongozwa na mwenyeji wake Mkurugenzi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Reli , Mhandisi Felix Nlalio (wa pili kushoto), kutembelea ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa –SGR, kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro.
Mkurugenzi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Reli, Mhandisi Felix Nlalio, akitoa maelezo ya ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa-SGR kwa kipande cha kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia- WB, Kanda ya Afrika, Bi. Anne Kabagambe, (katikati), alipofanya ziara katika miundombinu hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia- WB, Kanda ya Afrika, Bi. Anne Kabagambe, (wa pili kulia), akiipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wamiundombinu ya Reli ya Kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa-SGR, kwa fedha zake za ndani, wakati alipofanya ziara katika miundombinu hiyo, kushoto ni Mkurugenzi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Reli , Mhandisi Felix Nlalio.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia- WB, Kanda ya Afrika, Bi. Anne Kabagambe, (kushoto), akizungumza jambo na msaidizi wake, wakati wa ziara yake ya kutembelea ujenzi wa miundombinu ya Reli ya Kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa –SGR, kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro.
Muonekano wa moja ya Kituo cha Treni katika mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Reli ya Kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa –SGR, kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro.
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika, Bi. Anne Kabagambe, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutekeleza Mradi Mkubwa wa Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR) kwa kutumia fedha zake za ndani.
Bi. Kabagambe anayewakilisha nchi 22 za Kanda ya Afrika katika Benki hiyo yenye Makao yake Makuu Washington DC nchini Marekani, ametoa kongole hiyo kwa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, baada ya kutembelea na kukagua sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya Reli hiyo, kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro.
Alisema kuwa amefurahishwa na kiwango cha kiufundi kilichotumiwa na Kampuni ya Yapi Merkez iliyopewa kandarasi ya kujenga Reli hiyo na kwamba mradi huo sit u utakuwa na manufaa kwa Tanzania peke yake bali katika ukanda wa nchi za Afrika ambazo hazipakani na bahari.
“Nimekuja kujionea hatua kubwa zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania kujenga Reli hii ya kisasa na ninampongeza sana Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kwa kutekeleza mradi huu mkubwa na wa kielelezo kwa kutumia fedha zake za ndani” alisisitiza Bi. Kabagambe.
Aliahidi kuwa wakati Benki ya Dunia ikiangalia namna ya kuongeza ufadhili wa miradi kwa Tanzania, ataishawishi Benki hiyo pamoja na taasisi nyingine za Kimataifa zinazotoa misaada na mikopo kutoa fedha ili Tanzania iweze kutimiza malengo yake ya kukamilisha ujenzi wa Reli hiyo ambayo itafungua fursa za kiuchumi na kijamii katika ukanda wa Afrika.
Mkurugenzi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Reli, Kutoka Kampuni ya Reli-TRC, Mhandisi Felix Nlalio, aliezea kufurahishwa kwake na ziara ya kiongozi huyo wa Benki ya Dunia pamoja na ahadi aliyotoa ya kuipigia debe Serikali kwenye taasisi za kimataifa ili zitoe fedha za kukamilisha mradi huo.
Aliahidi kuwa kazi yao kubwa kama Kampuni ya Reli na Serikali kwa ujumla ni kuchapa kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kuwa ujenzi wa reli hiyo unaokwenda kwa kasi uweze kukamilika kwa wakati na kuiletea faida nchi pamoja na nchi jirani.
Ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa unaohusisha awamu mbili, Kipande cha kwanza kati ya Dar es Salaam na Morogoro (kilomita 300), ambacho kilianza kujengwa Mei 2, 2017 na kitakamilika ifikapo Novemba 2, 2019 kwa gharama ya Sh trilioni 2.7, wakati kipande cha pili kinachoanzia Morogoro –Makutupora (Manyoni, Singida) (kilomita 422), kilianza kujengwa Februari 26, 2018 na kitakamilika baada ya miezi 36 yaani Februari 25, 2021 kwa gharama ya Sh trilioni 4.4.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza mapato katika Bandari ya Dar es Salaam na pia kutaimarishara biashara hususani kati ya Tanzania na nchi zinazopitiwa na ushoroba wa kati (Central Corridor) za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Uganda na Rwanda.
0 Comments