Muuguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Rither Msuya (kulia) akichukua sampuli kwa ajili kupima damu ili kugundua Virusi vya Homa ya Ini. Hospitali ya Mloganzila leo imewapima na kutoa chanjo ya Homa ya Ini kwa wafanyakazi wake
Muuguzi Magreth Zacharia (katikati) akimpatia chanjo ya Homa ya Ini mtumishi wa Muhimbili-Mloganzila, kushoto ni muuguzi Sarah Igira.
Wataalam wa Maabara Muhimbili-Mloganzila wakiendelea na zoezi la upimaji na utoaji wa majibu ya Virusi vya Homa ya Ini (Hepatitis).
Baadhi ya watumishi wa Hospitali ya Mloganzila wakisubiri kupata huduma ya chanjo ya Homa ya Ini hii leo. 


Na Neema Wilson Mwangomo


Hospitali ya Taifa Muhimimbili-Mloganzila leo imetoa chanjo ya Homa ya Ini (Hepatitis) kwa wafanyakazi wake kwa lengo la kuwakinga watoa huduma mahala pa kazi ili wawe salama kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa.


Akizungumzia zoezi hilo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba MNH-Mloganzila Dkt. Mohamed Mohamed amesema dhamira ya hospitali ni kuhakikisha watumishi wake wote wanapatiwa chanjo hiyo muhimu.

“Zoezi linalofanyika hapa ni kupima kwanza Virusi vya Homa ya Ini kisha kutoa chanjo, lengo ni kuwapatia chanjo watumishi wote wa hospitali hii”amesema Dkt. Mohamed.

Ugonjwa wa homa ya Ini (Hepatitis) unasababishwa na virusi viitwavyo “Hepatitis B na C” na maambukizi ya ugonjwa huu yanashabiana na njia ya maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi kama vile kufanya ngono zisizo salama, kuchangia sindano au vikatio, kupewa damu isiyo pimwa, kupitia uzazi wa mama na mtoto hasa wakati wa kujifungua.

Ugonjwa huu sugu wa homa ya ini hauna tiba ya kuponya, isipokuwa dawa zilizo patikana hadi sasa zinaweza kupunguza kasi ya maambukizi mwilini na kuzuia madhara zaidi kwenye ini.

Ugonjwa huu unaweza kumpata mtu na kusababisha maradhi mwilini pasipo kuwa na dalili za aina yoyote ingawa kuna baadhi ya waathirika hupata dalili kama vile njano ya macho, kichefuchefu, tumbo kuuma kutapika na kuharisha kwa muda mfupi, mwili kuwashwa au kupata mkojo wa njano nyingi.