Serikali ya Tanzania imesaini mkataba na kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Airbus, kununua ndege mbili aina ya Airbus A220-300.
Mkataba huo umesainiwa leo, Septemba 19, 2019 kati ya Makamu wa rais wa kampuni hiyo Afrika, Hadi Akoum na upande wa Serikali ya Tanzania imewakilishwa na ofisa Mtendaji Mkuu wa wakala wa Ndege za Serikali, Benjamin Ndimila.

Muwakilishi huyo wa serikali ya Tanzania, bwana Ndimila amewaambia waandishi wa habari kuwa ndege hizo zitakuwa za kihistoria na ziko tofauti na ndege ambazo tayari shirika la ndege la Tanzania ATCL ilizozinunua awali.
Aidha hakutaja kiwango cha fedha kilichotolewa katika manunuzi hayo ya ndege mpya za Airbus A220-300 .
Kwa upande wake Akoum, alidai kuwa utengenezaji wa ndege ya aina hiyo unachukua mwaka mmoja hadi mwaka mmoja na nusu kukamilika kutokana na oda kuwa nyingi.
NDEGEHaki miliki ya pichaIKULU

Mambo muhimu kuhusu Airbus A220-300

Ndege hii ina urefu wa ni mita 38.7, na kwa jumla inaweza kuketi abiria 141.
Urefu wake kutoka chini kwenda juu ni mita 11.5, na upana wa mabawa yake ni mita 35.1.
Airbus 220-300 inaweza kusafiri umbali wa 5,920km safari moja, na inaweza kupaa ikiwa na uzani wa tani 67.6, na kutua ikiwa na uzani wa tani 58.7.
A220-300 ndiyo ndege kubwa miongoni mwa ndege za familia ya A220 na iliundwa kulenga soko la safai za ndege zinazowabeba abiria kati ya 130-160.
Ni ndege ambayo imeundwa kupunguza gharama ya matumizi yake ya mafuta kwa kila safari na pia kuwa yenye uwezo wa juu.
Injini zake zimepunguza matumizi ya mafuta kwa kila abiria kwa asilimia 20 ukilinganisha na ndege za awali za aina yake.
Ndege za A220 zimejengwa kwa vipande vinavyoweza kutengenezwa kwa haraka kiwandani iwapo vitahitajika wakati wa ukarabati.
Injini zake pia huwa za familia moja. Marubani waliozoea ndege aina ya A220-300 na A220-100 hawahitaji mafunzo zaidi kuweza kuziendesha.

Airbus A220-300 ina utofauti gani na Bombardier?

Rais Magufuli akiwa ndani ya ndege ya DreamlinerHaki miliki ya pichaIKULU
Ndege za Airbus A220 zilikuwa zinafahamika kama Bombardier CS100s kabla ya Airbus kuununua mradi huo wa utengenezaji wa ndege za C Series.
Ununuzi huo ulifanikishwa kupitia mkataba wa kibiashara kati ya kampuni ya Airbus na kampuni nyingine mbili: Bombardier Inc na Investissement Québec ambao ulianza kutekelezwa 1 Julai, 2018.
Airbus sasa humiliki 50.01% yahisa katika ubia wa utengezezaji wa ndege hizo ambao kirasmi hufahamika kama C Series Aircraft Limited Partnership, huku Bombardier na Investissement Québec wakimiliki takriban 34% na 16% ya hisa mtawalia.
Makao makuu ya mradi huo wa utengenezaji wa ndege pamoja na karakana zake vyote vinapatikana Mirabel, Québec.
Kutokana na ushirikiano huo, na hali kwamba Airbus inamiliki hisa nyingi, mradi wa C Series huhesabiwa sasa kuwa chini ya Airbus.

Air Tanzania ina ndege ngapi?

Shirika la Air Tanzania kwa sasa lina ndege saba, baada ya kununuliwa ndege sita chini ya mpango wa kufufua shirika hilo lililoanzishwa mwaka 1977.
Kuna Bombardier DASH8 Q400 tatu, mbili ambazo zilifika Tanzania Septemba 2016 na moja Juni 2017; Bombardier CS300 mbili na Boeing 787 Dreamliner ambazo zilitua Tanzania kati ya mei na Julai 2018.
Shirika hilo lilikuwa na Bombardier DASH8 Q300 moja ambayo ilikuwa ikihudumu tangu 2011.