Iran imeitungua kimakosa ndege ya Ukraine siku ya Jumatano, vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti.
Maafisa wa serikali ya Marekani kwa mujibu wa runinga ya CBS wanaamini ndege hiyo ilidunguliwa na kombora na kuiangusha karibu na Jiji la Tehran na kuua watu wote 176 waliokuwa ndani yake.

Ukraine awali ilisema kuwa inachunguza endapo ndege yake iliangushwa na kombora, jambo ambalo mamlaka za Iran zilikanusha vikali.
Kuanguka kwa ndege hiyo kulitokea saa chache baada ya Iran kushambulia kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq kwa makombora ya masafa marefu.
CBS imevinukuu vyanzo vya kijasusi vya Marekani vinavyodai kuwa picha za satelaiti zinaonesha mwanga wa makombora mawili ambao ulifuatiwa na mwanga wa mlipuko.
Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Alhamisi alisema: "nina mashaka" juu ya (kuanguka) kwa ndege. "Inawezekana kuna mtu amefanya kosa kubwa."
Iran imetangaza kutokabidhi kisanduku cheusi cha kuhifadhi taarifa za ndege kwa kampuni ya ndege ya Boeing ama serikali ya Marekani kwa uchunguzi wa ajali hiyo.
Hatua hiyo inatokana na mzozo uliokomaa baina ya Marekani na Iran, hasa baada ya Trump kuagiza shambulio la anga lililomuua Jenerali wa Iran Qasem Soleimani Januari 3.