Na Said Mwishehe, Michuzi TV.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kuwafukuza uanachama Mbunge wake Anthony Komu pamoja na Joseph Selani kwa madai licha ya kujipotezea sifa ya uanachama wameendelea kutoa maneno ya kejeli na dharau dhidi ya Chama na viongozi wake.
Pia Chama hicho kimetangaza kuwafuta unachama Mbunge David Silinde na Mbunge Wilfred Rwakatare kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kuonekana kwenye vyombo vya habari na njia nyingine za mawasiliano kutoa maneno ya kashfa na kejeli kwa Chama hicho, hivyo Kamati Kuu ya Chama hicho imefikia uamuzi huo.
Akizungumza leo Mei 11, 2020, jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika amesema Kamati Kuu imeazimia Komu na Selasini imeazimia wafukuzwe uanachama.
"Pamoja na wabunge hao kuwa wamepoteza sifa za uanachama wa Chama hicho bado wameendelea kutoa kauli za kejeli, kashfa na kukiuka maagizo ya Chama.Hivyo uamuzi uliofikiwa ni kuwafukuza uanachama na Kamati Kuu imeagiza Katibu Mkuu wa Chama kuamuandikia barua Spika wa Bunge kumuelezea uamuzi huo.
"Niseme kwamba pamoja na kusema wamepoteza sifa ya uanachama wa Chama, kwasababu kwa mujibu wa Katiba ya Chama sifa za uanachama wa Chadema kwenye kifungu namba 5(1.5)kinazungumzia umuhimu wa mwanachama kufuata falsafa na Itikadi ya Chama lakini wabunge hao wameonekana kutofuata falsafa na Itikadi na Chadema na badala yake wamekuwa wakifuata Itikadi ya Chama kingine,"amesema Mnyika.
Wakati huo huo amesema Chama hicho kimeamua Mbunge David Silinde na Wilfred Rwakatare sio tu wamekiuka agizo la Chama bali wamekuwa wakijitokeza kwenye vyombo vya habari kutoa maneno ya kashfa na kejeli dhidi ya maagizo ya Chama na viongozi."Kamati Kuu imefikia uamuzi wa kuwafuta uanachama".
Mbali na kuwachukulia hatua wabunge hao, Mnyika amesema kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema Mariam Msabaha ameshiriki kikuka maagizo ya Chama na kwamba alitakiwa awe mfano lakini yeye amekwenda kinyume, hivyo amevuliwa nafasi zake zote ndani ya Chama na kubaki na ubunge na atatakiwa kujieleza kwanini asichukuliwe hatua zaidi kwa kukiuka maagizo.
Kuhusu wabunge wengine wa Chadema ambao wamekwenda kinyume na maagizo ya chama lakini hawajaonesha utovu wa nidhamu kwa kutoa kashfa kwa chama watatakiwa wajieleze kwanini wasichukuliwe hatua zaidi kwa kiuka maagizo.
Katika hatua nyingine, Mnyika amesema kuwa wabunge wengine wote ambao wamekubali kutekeleza maagizo ya Chama ya kuwataka kukaa karantini kama sehemu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona watatakiwa kuendelea kuwa karantini hadi pale siku 14 ambazo zimetolewa na Chama hicho zitakapokamilika.
Amesema baada ya siku hizo kumalizika watarudi bungeni lakini kulingana na hali halisi ya Corona kama hali itakuwa haiko vizuri Chama hicho kitatoa maelekezo kwa wabunge hao.
0 Comments