DAR: NI mateso na maumivu makali anayopitia Amina Mohamedi Mwiru (32) mkazi wa Mbagala Kiburugwa ambaye amepatwa na tatizo la tumbo kujaa maji tangu alipojifungua Oktoba, mwaka jana.
Akizungumza na RISASI, Amina alisema baada ya kujifungua katika Zahanati ya Mbande, tumbo lilianza kujaa maji bila kufahamu chanzo chake.


“Nilipata ujauzito nikiwa na afya njema kabisa, sasa ilipofika Oktoba nikaenda hospitali nikajifungua salama, lakini ghafla nikaanza kuumwa na tumbo likaanza kujaa maji.
“Ikabidi nihamishiwe Hospitali ya Mbagala. Pale nilihudumiwa sikupata nafuu, ndipo nikapelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo nilipelekwa kwenye vipimo ambavyo nilikuwa nalipa Sh 100,000 na kuna vingine Sh 150,000.

“Madaktari waliniambia ini limesogea, mara wakaniambia ini lina kovu, kwa hiyo mpaka sasa sijajua tatizo linalonisumbua hasa ni nini. Kuna vipimo vingine nilitakiwa kupima, lakini sasa uwezo sina nimeuza hadi vitu ndani ili niweze kupata matibabu, lakini imeshindikana,” alisema.

Alisema maji huwa yanajaa tumboni mwake na kila anapoenda hospitali hutolewa maji hayo, lakini sasa hana uwezo wa kwenda tena.
“Huko hospitali sina uwezo wa kwenda tena maana ninapata maumivu makali, sina usafiri ambao utanifikisha huko na siwezi kukaa kwenye daladala kutokana na ugonjwa huu ambao sasa nimevimba tumbo na miguu, ambapo siwezi kutembea.

“Tangu nimejifungua Oktoba mpaka sasa, ninapata maumivu makali, huwa sipati hata usingizi. Natamani japo siku moja maumivu yapungue nipate hata usingizi kidogo tu.

“Kwa hiyo, ninawaomba Watanzania wenzangu wanisaidie ili niweze kwenda kumalizia vipimo na kufanyiwa matibabu nipone na kuendelea na vibiashara vyangu vidogovidogo maana nina familia ambayo inanitegemea,” alisema.

Akizungumzia na RISASI mume wa Amina, Baraka Issa, alisema alikuwa akifanya biashara ndogondogo kama machinga lakini mtaji wote shilingi milioni moja uliisha kwa ajili ya kumhudumia mkewe.

“Nimehangaika sana na mke wangu lakini kwa kweli nimekwama, naomba Watanzania watusaidie. Kama unavyoona sina ujanja tunaishi kwa kuungaunga tu na sijui hatma ya mke wangu,” alisema.

Kwa yeyote ambaye ameguswa na anaweza kumsaidia mama huyu kwa kutuma mchango wake kwenda namba 0712818160, jina Amina Mwiru.
Kusikiliza na kuona kwa undani wa tukio hili, ingia kwenye mtandao wa YouTube, tafuta Globa TV Online.

STORI: NEEMA ADRIAN, RISASI