Rais mstaafu wa serikali ya awamu ya tatu nchini Tanzania Benjamin William Mkapa amefariki akiwa na miaka 81.
Rais John Pombe Magufuli ametangaza usiku wa kuamkia leo Ijumaa kupitia runinga ya taifa taarifa za kufariki dunia kwa kiongozi huyo wa awamu ya tatu katika hospitali moja jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu.
Rais Magufuli alisema Bw. Mkapa amekuwa akipokea matibabu katika hospitali moja jiji Dar es Salaam, na kuongeza kuwa maelezo zaidi yatatolewa baadae.
''Mzee Benjamin William Mkapa Rais wa awamu ya tatu amefariki. Amefariki kwenye hospitali mjini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa. Niwaombe watanzania tulipokee hili. Taifa limepata msiba mkubwa. Tuendelee kumuombea Mzee wetu Rais Benjamin William Mkapa ambaye ametangulia mbele ya haki," ametangaza rais Magufuli.
mkapa
Taarifa hiyo hata hivyo haikuweka wazi Mzee Mkapa alikuwa akisumbuliwa na maradhi gani.
Katika ukurasa wake rasmi wa mtandao wa Twitter rais Magufuli amemuomboleza Mkapa na kusema atamkumbuka "kwa mapenzi yake makubwa kwa Taifa, ucha Mungu, uchapakazi na utendaji wake katika kujenga uchumi."
Taarifa zaidi juu ya msiba huo na mipango ya mazishi zinatarajiwa kutolewa baadae hii leo.
Mzee Mkapa alizaliwa Novemba 1938, Mkoani Mtwara kusini mwa Tanzania, na aliliongoza taifa hilo kwa mihula miwili toka mwaka 1995 mpaka 2005.