Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka wananchi kuchagua viongozi wenye sifa, kwa kuangalia utendaji kazi wao na sio wababaishaji ili waweze kukisaidia chama hicho kupata ushindi.

Shein ameyasema hayo leo Julai 19, 2020 wakati akihutubia mkutano wa kumtambulisha mgombea Urais Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi katika eneo la Kibirizi Kisiwani Pemba, ambapo amewaomba wananchi hao kuchagua viongozi makini watakaoweza kufanya kazi na mgombea huyo.


“Uchaguzi wa Chama wa kuteua viongozi unaanza kesho wachagueni hao vijana wenye uwezo na sio kwa kuwapendelea ili waisadie CCM ipate ushindi, tunataka safari hii Pemba tuoneshe mfano”, – amesema Dkt. Shein.

Aidha Dkt. Shein amesema kuwa chama hicho kinahitaji viongozi waadilifu katika nafasi za ubunge na udiwani na sio wenye tamaa ambao wataweza kumsaidia Dkt. Hussein Mwinyi katika kutimiza majukumu yake katika nafasi ya Urais.

Pia amedai kuwa Ushindi kwa Chama hicho ni lazima na kwamba wanahitaji viongozi watakaosaidia kukijenga chama hicho.