Vyuo vikuu vya harvard na MIT vinawafunza wanafunzi wake kupitia mtandaoni
Serikali ya Marekani chini ya uongozi wa rais Trump imefutilia mbali mipango yake ya kuwarudisha makwao wanafunzi wa kigeni ambao masomo yao yanaendelea kupitia mitandao kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.
Mabadiliko haya yanajiri wiki moja baada ya kutangazwa kwa sera hiyo.
Taasisi ya technolojia ya Masachussets MIT na chuo kikuu cha Havard kiliishtaki serikali kufuatia mpango huo.
Jaji wa wilaya Allison Burroughs mjini Masachussets amesema kwamba pande zote mbili zimeafikiana.
Makubaliano hayo yanarudisha sera ilioidhinishwa mwezi Machi , kufuatia mlipuko wa corona, ambayo inaruhusu wanafunzi wa kigeni kuhudhuria masomo yao kupitia mtandao na kusalia nchini humo kwa kutumia visa ya masomo kulingana na gazeti la New York Times.
Idadi kubwa ya wanafunzi wa kigeni husafiri kuelekea nchini Marekani kila mwaka na hupatia vyuo vikuu nchini humo pato kubwa.
Harvard ilitangaza hivi majuzi kwamba kutokana na hofu ya kusambaa kwa virusi vya corona, masomo yatatolewa kupitia mitandaoni wakati wanafunzi watakaporudi shule.
MIT kama taasisi nyengine za masomo imesema kwamba itaendelea kutoa masomo kupitia mtandao.

Je sera hiyo ilikuwa inasema nini?

Wanafunzi wa kigeni waliambiwa wiki iliopita kwamba hawataruhusiwa kusalia nchini Marekani wakati huu wa msimu wa vuli la sivyo wafanye kozi ya masomo ya kibinafsi.
Rais Trump amekuwa akiwasukuma wanafunzi wa vyuo vikuu na wale wa shule kurudi madarasani katika muhula mpya.
Maelezo ya picha,
Rais Trump amekuwa akiwasukuma wanafunzi wa vyuo vikuu na wale wa shule kurudi madarasani katika muhula mpya.
Wale ambao walirudi katika mataifa yao wakati muhula ulipokwisha mwezi Machi huku mlipuko wa corona ukizidi kuongezeka - waliambiwa kwamba hawataruhusiwa kurudi iwapo masomo yao yatakuwa yakiendelea kupitia mtandao.
Shirika la uhamiaji na forodha nchini humo ICE lilikuwa limesema kwamba raia watarudishwa makwao iwapo hawataafikia sheria hiyo.
Mipango ya kubadilishana wanafunzi ambayo husimamiwa na ICE ilikuwa imewaruhusu wanafunzi wa kigeni kuendelea na masomo yao ya mtandao wakati wa msimu wa joto na baridi mwaka 2020 huku wakisalia nchini humo.
Lakini mnamo mwezi Julai kitengo hicho kilisema kwamba wanafunzi wa kigeni ambao watafeli kufanya masomo ya kujifunza binafsi watakabiliwa na sheria hizo za uhamiaji.
Je vyuo vikuu vilipokeleaje wito huo?
Siku mbili baadaye , Harvard na MIT ziliwasilisha kesi mahakamani zikitaka kubadili msimamo huo wa serikali wakidai kuwa agizo hilo ni ukiukaji wa sheria usiostahiki na matumizi mabaya ya busara.' Makumi ya vyuo vingine pia yaliunga mkono kesi hiyo.
Kinachowapatia shinikizo , vilisema vyuo hivyo 59 vikiunga mkono kesi hiyo , "hakuna uhusiano wowote na kuhakikisha kwamba wanafunzi wanajihusisha na" kozi kamili ya masomo "au kulinda uaminifu wa mpango wa visa wa wanafunzi. Badala yake, kusudi lake .. . ni 'kuhamasisha shule kufunguliwa tena. "
Rais Trump amekuwa akiwasukuma wanafunzi wa vyuo vikuu na wale wa shule kurudi madarasani katika muhula mpya.
Anadhania kwamba kufunguliwa kwa shule kutaashiria kuimarika kwa uchumi kufuatia miezi kadhaa ya machafuko, hatua ambayo inaweza kumfaidi katika kampeni yake katika kuchaguliwa kwa kipindi kipya cha miaka minne kama rais mwezi Novemba.
Hatahivyo walimu wengi wana wasiwasi kuhusu ustawi wa wanafunzi na wanataka kuendelea kutekeleza sheria ya kutokaribiana huku mlipuko huo ukiendelea.
Je ni visa gani zilizoathirika?
Sera hiyo iliwaathiri wamiliki wa visa za F-1 na M-1 visas, ambazo ni za wanafunzi wa kitaaluma na wa ufundi.
Idara ya masuala ya kigeni ilitoa Visa 388,839 aina za F na 9,518 aina ya M katika mwaka wa 2019 kulingana na takwimu za shirika hilo la uhamiaji,
Kulingana na idara ya biashara nchini Marekani , wanafunzi wa kimataifa walichangia $45bn (£36bn) katika uchumi wa taifa hilo 2018.