Uhusiano kati ya Rais Uhuru na naibu wake Uhuru Ruto ndani ya chama tawala cha Jubilee umekuwa ukidorora

Baada ya kuchaguliwa tena kuongoza kwa miaka mitano, jambo ambalo lilitokea baada ya kufutiliwa mbali kwa uchaguzi wao na mahakama, Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wamekuwa wakivuta kuelekea pande mbili tofauti.

Kutengana kwao kulianza kuonekana baada ya mwezi wa Machi, 2018,(Rais Kenyatta alianza kuwa na uhusiano na kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga) na baada ya hapo, kumekuwepo na shutuma kutoka pande mbili husika.

Rais Kenyatta alimshutumu naibu wake kwa kushiriki katika kampeini za kisiasa za kumrithi mapema mno badala ya kulenga miradi waliyokuwa wameahidi Wakenya. Kwa upande mwingine, naibu Rais William Ruto anaiona hatua hii kama njama ya kumkata mikono katika kumrithi rais Uhuru na kwenda kinyume cha makubaliano yao ya mwaka wa 2013 ambayo yalifanywa wakati wawili hao walikuwa wameshtakiwa kwa makosa ya jinai katika mahakama ya kimataifa(ICC).

Katika chama cha Jubilee, uhusiano kati ya Rais Uhuru na naibu wake umekuwa unadorora. Chama cha Jubilee ambacho kiliundwa mnamo Septemba 2016 ili kuunda muungano kati ya Uhuru Kenyatta na Ruto sasa unadhibitiwa na Rais Kenyatta huku viongozi wake wengine wakuu, akiwemo Bw. Ruto wakiwa wameonekana kutengwa.

Uhusiano wa karibu wa Rais Kenyatta na Raila Odinga unadaiwa kuwa chanzo cha kutengwa kwa William Ruto
Maelezo ya picha,

Uhusiano wa karibu wa Rais Kenyatta (kushoto) na Raila Odinga unadaiwa kuwa chanzo cha kutengwa kwa William Ruto

Hali hii inatokana na siasa za ndani kwa ndani kwenye chama hicho tawala kuhusiana na suala la vita dhidi ya ufisadi, huku Rais Kenyatta akikumbwa na mgawanyiko katika siasa za Mlima Kenya, anakotoka Rais Kenyatta. Wafuasi wa Rais Kenyatta wamegawanyika; wengine wakimuunga mkono Bw. Ruto huku wengine wakimuunga mkono Rais Kenyatta.

Haya yakiendelea, wanachama wa chama cha upinzani Orange Democratic Movement (ODM) wamekuwa wakimtetea Rais Kenyatta kutokana na shutuma za wanajubilee. Kwa njia hii, Raila Odinga amekuwa mtetezi wa Rais Kenyatta huku Ruto akionekana kuongoza upinzani ndani ya chama tawala cha Jubilee.

Kwa upande wake, Rais Kenyatta ameunda muungano mpya akitumia wapinzani wa kisiasa wa Ruto akimleta karibu kiongozi wa upinzani Raila Odinga wa chama cha Orange Democratic Movement(ODM), kinara wa Wiper Democratic Movement (WDM) Kalonzo Musyoka, Gideon Moi wa Kanu na Isaac Ruto wa Chama Cha Mashinani.

Ushirikiano huu na vyama vingine umesababisha fujo katika vyama vya upinzani nchini Kenya huku vyama vingine vikijaribu kusimama imara hasa katika ngome zao za kisiasa. Kwa mfano chama cha Ford-K kimekumbwa na migogoro ya kiusimamizi ya ndani kwa ndani na mpaka sasa kina viongozi wawili. Makundi mawili ya uongozi sasa yako mahakamani kupigania uongozi wa chama cha Fork-K.

Hali hii ndiyo iliyopelekea Rais Kenyatta kuchukua usimamizi dhabiti wa bunge la kitaifa na lile la seneti ambapo kwa sasa mabunge haya hayana upande wa upinzani. Naibu wa Spika wa bunge la seneti, kiongozi wa wengi na kamati zake zimefanyiwa mabadiliko makubwa. Hali hii imekumba bunge la kitaifa ambapo kiongozi wa wengi na naibu wake na kamati zake pia zimefanyiwa mchujo. Hali hii mpya inatishia uhuru wa bunge katika utendakazi wake nchini Kenya.

Kalonzo Musyoka
Maelezo ya picha,

Rais Kenyatta anadaiwa kuwaleta karibu wapinzani wa Ruto akiwemo kinara wa Wiper Democratic Movement (WDM) Kalonzo Musyoka

Miungano mipya katika siasa za Kenya ina misingi yake katika uhusiano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga na huenda pia ikakumbwa na mitetemeko zaidi huku viongozi hawa wawili wakiweka mipango kwa kura ya maamuzi kuhusu katiba ya Kenya. Kampeini kuhusiana na jambo hili zilisambaratishwa na ugonjwa wa Covid-19 huku Rais Kenyatta na Raila Odinga wakisisitiza siku za hivi karibuni kuwa bado mipango ingalipo.

Kwa naibu Rais William Ruto, kuondolewa kwa wandani wake katika nyadhifa mbali mbali kunamaanisha kuwa ni bayana kwamba makubaliano yake na Rais Kenyatta ya mwaka wa 2013 ambayo yangemfanya kumrithi Kenyatta kama rais wa tano wa Kenya, hayapo tena. Haya yakimaanisha kuwa ni lazima bwana Ruto apange mkakati mwingine.

Ni bayana pia kwamba huenda akafaidika kutokana na kutoelewana kwa kundi kubwa lililoletwa pamoja na Rais Kenyatta. Mgogoro na uhusiano baina ya Rais Kenyatta na naibu wake huenda ukachacha zaidi iwapo mpango wa marekebisho ya katiba utaanza hivi karibuni. Bwana Ruto anatofautiana na Rais kuhusiana na jambo hili. Ruto anasema kwamba hakuna dharura katika kuifanyia marekebisho katiba ya Kenya na kwamba fikra ya kutaka kuipanua serikali hasa katika ngazi na nyadhifa za juu kupitia kwa marekebisho haya ni jambo lisilofaa.

Wengi wanaamini kwamba Ruto amekasirishwa na kuvunjwa moyo baada ya kugundua kwamba Rais Kenyatta huenda asimuunge mkono katika uchaguzi wa 2022. Hali hii imepelekea maswali mengi kuibuka kama chama cha Jubilee kitakuwa imara hadi uchaguzi wa mwaka wa 2022. Kumekuwepo na minongono kwamba Bwana Ruto huenda akakihama chama hicho ambacho amedai hakina udhabiti na kimetekwa nyara na matapeli wa kisiasa.

William Ruto
Maelezo ya picha,

Wengi wanaamini kwamba Ruto amekasirika baada ya kugundua kwamba Rais Kenyatta huenda asimuunge mkono katika uchaguzi wa 2022

Bwana Ruto amedokeza pia kuwa huenda akaongoza upande utakaopinga kura ya maamuzi kuhusu katiba ya Kenya huku akikejeli wanaounga mkono suala hili. "Hata sijui ni nini kitakachobadilishwa…kulingana na ufahamu wangu, mabadiliko haya yanasukumwa na viongozi, si wananchi. Wananchi kwa sasa wanashughulishwa na ukosefu wa ajira, na mambo mengine ya kimsingi katika maisha yao." Bwana Ruto amenukuliwa akisema.Kwa upande wake, Rais Kenyatta anasisitiza kwamba kura ya maamuzi ni lazima kufanyika ili kuondoa hali ya wasiwasi ambayo hukumba Kenya kila mara kabla na baada ya uchaguzi mkuu kwa sababu wa jamii fulani "kuhisi kutengwa kutoka kwa uongozi wa taifa" jambo linalopelekea uhasama baina na kati ya jamii.

Rais Kenyata amekuwa akieleza kuwa ana maono ya kulipokeza taifa hali ya mshikamano na umoja kupitia mchakato wa BBI, ambao utakuwa sehemu ya jinsi atakavyokumbukwa akiondoka mamlakani.

Lakini naibu wake anahoji kuwa mabadiliko ya kikatiba hayawezi kufanywa kuwa jinsi kiongozi yeyote atakavyokumbukwa. "Mabadiliko ya kikatiba si jambo tunaloweza kuamua kama chama- ni kwa Wakenya wote kuamua. Si jambo ambalo ninaweza kusema kwamba nitakumbukwa kwa kubadilisha katiba," aliambia kituo kimoja cha televisheni nchini Kenya hivi maajuzi.

Unaweza pia kusoma:

Itakumbukwa kwamba mnamo mwaka wa 2005, Rais Mstaafu Mwai Kibaki aliwatimua Raila Odinga na wandani wake kwa kuongoza upinzani dhidi ya katiba iliyopendekezwa wakati huo. Hata hivyo, kulingana na katiba ya Kenya ya sasa, Rais Uhuru hana uwezo wa kumtimua naibu wake kutoka wadhifa wake. Hata hivyo, Rais Kenyatta anaweza kuchukua hatua na kufanya mabadiliko katika serikali kwa jumla na kumpunguzia uwezo wake. Rais pia anaweza kuanzisha mswaada wa kutokuwa na Imani na naibu wake bungeni.

Kwa miezi kadhaa, Bwana Ruto amekwepa kumshutumu Rais Kenyatta hadharani lakini siku za hivi karibuni yeye na wandani wake wanaonekana kumshutumu Rais Kenyatta moja kwa moja hadharani. Kwa mfano, wabunge wawili ambao ni wandani wa Bwana Ruto wametoa matamshi ya kumshutumu Rais Kenyatta na mamake, Ngina Kenyatta, kwa masaibu yanayokumba Kenya. Wabunge hao, Oscar Sudi na Johanna Ngeno tayari wameshikwa na kufunguliwa mashtaka. Aidha, wabunge wengine na wandani wa bwana Ruto wameanza kufuata mkondo huo siku za hivi karibuni jambo ambalo linaonyesha kuwa Bwana Ruto yuko karibu kuondoka serikalini na kulenga kampeini zake za mwaka wa 2022.

Wengi wanaamini kwamba msukosuko uliopo katika chama cha Jubilee na uhusiano unaoendelea kudorora baina ya Rais Kenyatta na naibu wake ni mipango ya bwana Ruto ya kuondoka kwenye serikali na kulenga kampeini zake za mwaka wa 2022 huku kura ya maamuzi inayotarajiwa kuhusu katiba ikimpa nafasi nzuri ya kufanya hivi.

Katika siku za hivi karibuni, Bwana Ruto amekuwa akifanya mikutano nyumbani kwake na mingine katika maeneo mbali mbali nchini Kenya ambapo amechagia mamilioni kwa vijana na makundi ya akina mama.

Pia, amekuwa na mikutano na viongozi mbali mbali wa makanisa na washawishi wengine akionekana kupanga kampeini zake bila kumtegemea Rais Kenyatta. Aidha, baadhi ya viongozi wanaomuunga mkono Bw. Ruto wamekuwa wakimrushia cheche za maneno Rais Kenyatta wakimshutumu kwa kumtenga kutoka shughuli muhimu za chama cha Jubilee, serikali, na kutomuunga mkono naibu wake kisiasa.

Kwa upande mwingine, Bwana Ruto ameshutumiwa na baadhi ya wanasiasa ambao wanatilia shaka ukosoaji wake wa serikali ambayo bado yeye ndiye naibu wa Rais.

Kilicho wazi katika siasa za Kenya kwa sasa ni kuwa uhusiano baina ya Rais Kenyatta na naibu wake katika chama tawala cha Jubilee na serikali kwa jumla unakumbwa na wakati mgumu hasa nchi inapojishughulisha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022 huku kila mmoja akivutia kwake.

Prof Mogambi ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi: barua pepe:hmogambi@yahoo.co.uk