Rais mteule wa Tanzania John Pombe Magufuli hatimaye amepokea cheti cha ushindi wake katika uchaguzi wa urais uliokamilika .

Jaji mstaafu na mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Semistocles Kaijage aliwakabidhi rais Magufuli na makamu wake Samia Hassan Suluhu vyeti hivyo kufuatia ushindi mkubwa wa chama tawala cha CCM, uchaguzi ambao umepingwa na vyama vikuu vya upinzani.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa cheti hicho, Magufuli amesema kwamba ushindi alioupata ni deni kubwa kwa Watanzania huku akiwashukuru wapinzani wake kwa kumpatia ushindani mkubwa.

Kiongozi huyo amesema kwamba upinzani huo umesaidia katika kufahamu ni nini Watanzania wanataka.

''Nawashukuru pia na kuwapongeza kwa kukubali matokeo na kuja kushiriki hafla hii. Hii ni ishara ya kukomaa kwenu kisiasa - hongereni sana''.

''Ni kweli kwamba wananchi wametupatia ushindi mkubwa sana, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya kudharau maoni na ushauri wenu''.

Bwana Magufuli amewashukuru Watanzania kwa kukipa ushindi chama chake cha Mapinduzi (CCM) katika nafasi ya Urais, Ubunge na kule Zanzibar katika nafasi ya uwakilishi na nafasi ya Udiwani.

''Kupata asilimia 84.4 ni imani kubwa sana kwa Watanzania na nasema kwa dhati nina deni kubwa sana kwa Watanzania, imani yao nitaitimiza kwa kufanya kazi sana usiku na mchana'', Bwana Magufuli amesema.

magu

Bwana Magufuli hakusita kuwashukuru viongozi wa dini ambao kwa kipindi chote cha uchaguzi waliweza kuwaongoza kwa dua na sala na hatimae kumaliza uchaguzi kwa usalama na taifa lao kuendelea kubaki kwa amani.

''Navishukuru pia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kuhakikisha amani na usalama vinatawala katika kipindi chote cha uchaguzi,'' amesema Bwana Magufuli huku akielezea matumaini yake kuwa usalama utaendelea hata baada ya uchaguzi.

Pia Bwana Magufuli amesema kuwa uchaguzi umeisha na sasa ni wakati wa kufanya kazi.

"Siasa sio vita siasa sio ugomvi sisi sote ni Watanzania napenda kuwaahidi nitashirikiana nanyi katika kuhakikisha tunasukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. Tanzania kwanza mambo mengine baadae" Magufuli amesema.

Amewashukuru viongozi wa nchi nyingine waliomtumia salamu za pongezi.