Rais Uhuru Kenyatta ameondoa masharti ya kutotoka nje kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri nchini Kenya.

Akizungumza katika sherehe za kuadhimisha siku kuu ya mashujaa, Uhuru amesema kwamba hatua hiyo inafuatia kupungua kwa visa vya maambukizi nchini Kenya.

Amesema kwamba kufikia sasa ni watu milioni 5 waliopata chanjo ya ugonjwa wa corona na kuongezea kwamba serikali yake inaelekea kuafikia lengo lake la kuwapatia chanjo hiyo watu milioni 10 kufikia Disemba mwaka huu.

Hatahivyo rais Uhuru Kenyatta amewataka Wakenya kuchukua jukumu la kujilinda na kuwalinda wapendwa wao.

Hatua hiyo inajiri wakati ambapo Wakenya wamekuwa wakiitaka serikali kuondoa masharti hayo kwa lengo la kuendelea na biashara zao za kawaida.

Uhuru alisema kwamba baraza la viongozi wa kidini, wafanyakazi wa afya na maafisa wa usalama walifanya kazi nzuri katika kuhakikisha kwamba masharti ya kukabiliana na ugonjwa huo yanaheshimiwa.