Kijana wa Kitanzania aliyekuwa akiishi nchini Marekani na wazazi wake, Humphrey Magwira amepigwa risasi na kuuawa katika eneo la Fort Bend County, Houston katika Jimbo la Texas nchini Marekani.

 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka mamlaka husika, Humphrey ambaye alikuwa ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Houston, alifikwa na mauti Ijumaa, Oktoba 15, mchana jirani na makutano ya Barabara za Beechnut na Addicks Clodine.

 

Chanzo cha tukio hilo, kinaelezwa kuwa ni ajali ndogo iliyokuwa imetokea kwa magari mawili, likiwemo alilokuwa akiendesha marehemu Humphrey, kugongana katika eneo hilo.

 

Ndani ya sekunde chache, dereva wa gari la pili aliyetambuliwa kwa jina la Ramon Vasquez mwenye umri wa miaka 19, aliteremka na kufyatua risasi kadhaa, zilizomjeruhi vibaya kijana huyo.

 

Baada ya tukio hilo, askari wa uokoaji walimkimbiza Humphrey hospitali kwa kutumia helikopta lakini muda mfupi baadaye, madaktari walithibitisha kwamba tayari amefariki dunia.

 

Dereva huyo, baada ya kutenda unyama huo, alikimbia eneo la tukio kwa kutumia gari lake lakini saa 24 baadaye, Jumamosi asubuhi, polisi walifanikiwa kumkamata.

 

Akielezea tukio hilo, afisa wa polisi wa Fort Bend County aliyetambulika kwa jina moja la Fagan, amenukuliwa akisema tukio hilo la kushangaza, limesababishwa na ajali ndogo ya bahati mbaya na kusababisha kifo cha kijana huyo mdogo na kutoa pole kwa familia ya kijana huyo, huku akieleza kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi wao.

 

Kwa upande wa mama wa marehemu, Josephine Kuyangana, amenukuliwa akisema kwa uchungu kwamba ni tukio la kuhuzunisha sana na haamini kama hatamuona tena mwanaye huyo.

 

Inaelezwa kwamba takribani miaka nane iliyopita, Kuyangana na familia yake, walihamia Houston kwa ajili ya kutafuta maisha.

Inazidi kuelezwa kuwa, marehemu alihitimu masomo yake katika Shule ya Westside High School ambapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Houston, akisomea uhandisi wa kompyuta huku pia akicheza soka katika timu ya chuo hicho.

 

Tukio hilo limetokea mita chache kutoka nyumbani kwa familia hiyo na kwa mujibu wa mama wa marehemu, Humphrey alikuwa akielekea saluni kwa ajili ya kunyoa nywele.

 

Wakati polisi wakieleza kwamba mtuhumiwa bado anashikiliwa, kaka wa marehemu, Rodericque Magwira, amesema wanazo taarifa kwamba mtuhumiwa huyo ameachiwa kwa dhamana ya dola za Kimarekani 50,000 na kueleza kuwa familia yake imeshangazwa na kitendo cha polisi cha polisi kumuachia muuaji huyo.

 

“Kwa nini amepewa nafasi ya kurudi uraiani? Amemuua mdogo wangu bila ya sababu yoyote, haiingii akilini kabisa,” alinukuliwa kaka huyo wa marehemu huku akiiomba serikali kuingilia kati ili haki ya mdogo wake ipatikane.

 

Tayari Watanzania waishio nchini humo, wameanza harambee ya kuichangia familia hiyo kupitia mtandao wa GoFundMe, ili kuusafirisha mwili wa Humphrey kuja nchini Tanzania kwa mazishi.