Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kwa vyovyote itakavyokuwa ni lazima ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka jijini Dar es Salaam hadi mkoani Mwanza ukamilike kwa wakati na fedha zitakazotumika ni mikopo yenye masharti nafuu.
Rais Samia ameyasema hayo leo Desemba 28, 2021 Ikulu, Jijini Dar es Salaam wakati wa utiaji saini mkataba wa ujenzi kati ya Shirika la Reli la Tanzania (TRC) na Kampuni ya Yerpi Merkezi ya nchini Uturuki kwaajili ya ujenzi wa reli wa kipande cha kilometa 368 yenye gharama ya dola za kimarekani bilioni 1.908.
Samia amesema reli hiyo ina umuhimu mkubwa katika uchumi wa nchi kwa sababu itarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo ndani na nje ya nchi, hivyo lazima ijengwe kama ilivyokusudiwa bila ya kutumia kodi za wananchi.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amebainisha kuwa uwekezaji wa ujenzi wa vipande vinne kati vitano vya awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo umefikia Sh14.7 trilioni ukijumuisha na kodi na kwamba hatakubali fedha hizo zipotee bure kwa mradi kushindwa kukamilika.
"Tusipoendelea na reli hakutakuwa na faida, fedha tulizozilaza pale chini zitakua hazina maana," amesema Rais Samia na kusisitiza kuwa ni lazima Serikali ikope fedha nje kukidhi mahitaji ya mradi huo.
"Kwa hiyo kwa njia yoyote kwa vyovyote tutakopa, tutaangalia njia rahisi zitakazotufaa za kukopa kwa sababu fedha hizi hatutazitoa kwenye tozo wala kwenye kodi tunazokusanya ndani," amesisitiza Rais Samia.
Kuhusu kupata mkopo, Rais Samia amesema, "Niwaombe ndugu zangu mnaosimamia hii sekta twendeni, mimi niko pamoja nanyi tutasimama kuangalia mikopo inayotufaa tukiongozwa na Gavana wa Benki Kuu na Waziri wa Fedha yuko hapa atatuongoza mikopo gani itatufaa tutachukua tumalize reli hii muda uliopangwa ili iweze kutengeneza fedha tulipe mikopo tunayochukua."
Ukubwa wa reli hiyo
Mkandarasi huyo, Yerpi Markezi anajenga vipande vitatu kati ya vitano vya reli hiyo yenye mtandao usiopungua kilomita 2,561 ikiunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Katavi na nchi zisizokuwa na bandari (Rwanda, Burundi na Congo DRC).
Ameongeza kuwa tayari ameshaagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia TRC kukamilisha taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi kipande kilichobaki cha Tabora - Isaka na kipande kipya cha awamu ya pili kutoka Tabora hadi Kigoma.
Amesema, "Nitoe maelekezo kwamba tunapokwenda kumaliza (reli ya SGR) kipaumbele kitolewe kwa yale matawi yanayotuunganisha na nchi za jirani ili tuweze kurahisisha biashara zetu, kuingia kwenye masoko jirani."
Spika Ndugai 'Adai' nchi itapigwa mnada
Vyombo mbalimbali nchini Tanzania vimeripoti kuhusu hotuba ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai aliyehoji wanaofurahia nchi kukopa na kufikia deni la Sh 70 trilioni za kitanzania.
0 Comments